Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amemtaka mkandarasi anayejenga barabara mkoani Morogoro kufuata masharti ya mkataba la sivyo utavunjwa na kampuni hiyo kupigwa marufuku kupewa kazi yoyote nchini.
Mkandarasi huyo ni kampuni ya Henan Railway kutoka China anayejenga barabara ya Ifakara–Mbingu yenye urefu wa kilometa 62.5, ambapo ingawa tayari imelipwa malipo ya awali, kasi ya ujenzi haiendani na kiwango kilichotakiwa kufikiwa hadi sasa.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Ulega amesema Serikali haiwezi kuendelea kuvumilia ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya wananchi na maendeleo ya uchumi.
“Hivi hamuoni namna wananchi wanavyoumia kwa kutotimiza wajibu wenu kwa mujibu wa mkataba? Barabara haijengwi kwa kasi, vumbi ni jingi na usumbufu kwa wananchi ni mkubwa. Hili hatuwezi kuvumilia. Mkiendelea hivi itabidi tuchukue hatua ngumu,” alisema.
Waziri huyo ametoa muda wa wiki moja kwa wataalamu wa Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kukutana na uongozi wa juu wa kampuni hiyo katika kikao cha ngazi ya juu ili kujadili hatma ya utekelezaji wa mradi huo.
Waziri huyo amesema mradi huo umechelewa kukamilika kwa kiwango kikubwa, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia takribani asilimia tano pekee, licha ya Serikali kuwa tayari imelipa malipo ya awali ya shilingi bilioni 9.5. Amesema kiwango hicho cha fedha hakilingani na maendeleo halisi ya kazi yaliyopo eneo la mradi.
"Serikali haitakuwa tayari kuona fedha za umma zinatumika bila kuleta matokeo yaliyokusudiwa. Mkandarasi lazima aonyeshe uwezo na dhamira ya kukamilisha mradi huu, vinginevyo hatua stahiki zitachukuliwa," alisisitiza Ulega.
Pia ameeleza kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakamilika kwa wakati ili kuondoa adha wanazokumbana nazo wananchi kutokana na ubovu wa miundombinu, hali inayochangia ugumu wa usafiri na kuongezeka kwa gharama za nauli.
Aidha, Waziri Ulega amemuagiza mkandarasi kuanza mara moja kufanya uboreshaji wa barabara hiyo kwa kuziba mashimo na kumwaga maji mara kwa mara ili kupunguza vumbi linalowaathiri wananchi wanaoishi na kutumia barabara hiyo wakati ujenzi ukiendelea.
Katika hatua nyingine, Ulega ameagiza kipande cha barabara kinachoanzia Chita hadi kuunganisha na Mkoa wa Njombe kifanyiwe matengenezo ya haraka ili kiweze kupitika kwa urahisi katika kipindi chote cha mwaka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima ameeleza umuhimu wa barabara hiyo katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, mazao na abiria katika kuchochea uchumi wa wananchi hao huku akisisitiza kuwa barabara hiyo ni huduma muhimu inayogusa maisha ya ya wananchi wa Mlimba na Wilaya ya Kilombero.
Naye, Mbunge wa jimbo la Mlimba Rose Rwakatare amemuomba Waziri wa Ujenzi kumbana Mkandarasi ili aendeleze Ujenzi wa barabara kwa kasi kwani fedha aloyolipwa haiendani na kazi iliyofanyika.





No comments:
Post a Comment