WABUNIFU WA KITANZANIA KUONYESHA TEKNOLOJIA ZAO TANGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 30, 2026

WABUNIFU WA KITANZANIA KUONYESHA TEKNOLOJIA ZAO TANGA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametangaza maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa mwaka 2026, yatakayofanyika kuanzia Agosti 15 hadi 24 katika viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga.

Akitangaza maadhimisho hayo amesema yatawakutanisha wadau kutoka wizara mbalimbali, vyuo vya elimu ya juu, vyuo vya ufundi na ufundi stadi, mashirika ya utafiti na sekta binafsi kwa ajili ya maonesho na mijadala ya kimkakati katika kuimarisha elimu, ujuzi na ubunifu nchini.

Prof. Mkenda amebainisha kuwa wananchi watapata fursa ya kushuhudia bunifu zilizobuniwa na vijana wa Kitanzania, ambazo zikovkatika hatua mbalimbali ikiwemo zilizo sokoni akitoleta mfano mashine ya kukamua mafuta ya parachichi (Avomero), mabegi ya shule yenye mfumo wa umeme jua (Soma Bags), na mita janja za maji (Smart Prepaid Water Meter).

Amesisitiza kuwa bunifu hizo ni ushahidi wa jitihada za serikali kuendeleza wabunifu na kuwezesha uwepo wa bidhaa hizo za ndani zinazotatua changamoto za kijamii na kiuchumi.

Aidha, Waziri Mkenda amesema zaidi ya bunifu 70 zipo katika hatua mbalimbali za kukuzwa ili ziwe biashara halisi na kuchangia uchumi wa taifa. Ameongeza kuwa Serikali imeanzisha mfuko maalum wa kusaidia wabunifu kupunguza gharama za uzalishaji na kuharakisha ukuaji wa biashara zao.

Pia ameeleza kuwa katika wiki ya ubunifu kutakuwa na Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi ambapo ni vigego vyake vya ushindani ni vya kimataifa na ikiwa ni maandalixi ya Nchi kushiriki katika mashindano ya kimataifa (World Skills Competition)

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, amesema serikali ipo katika hatua za kuhuisha Sera ya Taifa ya Sayansi, Teknolojia ili iendane na mabadiliko ya kidunia na mahitaji ya sasa.

Ameeleza kuwa sera mpya itakuwa mwongozo wa namna masuala yote ya sayansi, teknolojia na ubunifu yatakavyoshughulikiwa nchini, ikiwemo mashindano ya kitaifa ya ubunifu.

Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Prof. Ladislus Mnyone, amesema serikali imekamilisha mkakati wa kuongeza ushiriki wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) katika kuendeleza bunifu na teknolojia za ndani.

Aidha, amebainisha kuwa katika kuendelea kuibua wabunifu halmashauri 90 tayari zimeanzisha madawati ya sayansi na ubunifu, hatua inayowawezesha wabunifu kuwasilisha mawazo yao na kuunganishwa na taasisi ya COSTECH kwa ajili ya urndelezaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amepongeza jitihada za serikali katika kuhamasisha ubunifu nchini. Amesema banda maalum litakuwepo Tanga kuonyesha bunifu zilizofanikiwa kuingia sokoni ili kutoa ushuhuda wa mafanikio ya wabunifu wa Kitanzania.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa serikali, wadau na wananchi ni muhimu katika kuendeleza ubunifu na kuchochea maendeleo ya taifa.

Kauli mbiu ya mwaka huu: “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”

No comments:

Post a Comment