TAMISEMI YAZINDUA UMOJA WA WATENDAJI KATA, VIJIJI, MITAA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 30, 2026

TAMISEMI YAZINDUA UMOJA WA WATENDAJI KATA, VIJIJI, MITAA


Na OWM – TAMISEMI, Dodoma


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Bw. Sospeter Mtwale, amezindua rasmi wa Umoja wa Watendaji Tanzania (UWATA) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe na kuutaka umoja huo kuimarisha utendaji kazi wa Watendaji Kata, Vijiji na Mitaa kwani ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika kutekeleza azma ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.


Naibu Katibu Mkuu, Bw. Mtwale, amezindua umoja huo wa Watendaji Tanzania (UWATA) leo Julai 30, 2026 katika Ukumbi wa Uriyo jijini Dodoma na kuutaka umoja huo kuwa chombo muhimu cha kuwezesha wananchi kupata huduma bora za kijamii katika ngazi ya kata, vijiji na mitaa kutoka Serikalini.

“Nawapongeza kwa kuunda chombo hiki muhimu sana ambacho kikitekeleza majukumu yake kwa ufanisi kitawezesha wananchi kupata tabasamu kama ambavyo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza watumishi wa umma kutimiza azma hiyo,” amesema Bw. Mtwale.

Bw. Mtwale amesisitiza kuwa, Serikali inaunga mkono uamuzi wa kuanzisha Umoja wa Watendaji Tanzania (UWATA) na kuwataka wanachama wa umoja huo kutumia kikao kazi hicho kujadili, kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za kutatua changamoto zinazokwamisha utendaji kazi wa Watendaji Kata, Vijiji na Mitaa katika kuwahudumia wananchi.

Bw. Mtwale ameutaka umoja huo wa UWATA kuhakikisha unasimamia utendaji kazi wa Watendaji nchini unajikita katika msingi ya Utawala Bora yaani kutenda haki, kufuata sheria, na kulinda rasilimali za umma, Uadilifu na uzalendo ili kuepuka rushwa na kulinda maslahi ya taifa katika maamuzi na utoaji wa huduma, pamoja na usimamizi wa miradi ya maendeleo na kufuata kanuni za manunuzi kwenye vituo na vijiji ili kufikia malengo ya Serikali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Watendaji Tanzania (UWATA) Bi. Victoria Malindila amesema kuwa uzinduzi wa umoja huo ni mwanzo wa safari mpya ya kuwaunganisha Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa ili kujenga utendaji kazi unaozingatia weledi, uwajibikaji, mshikamano na ubunifu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.

Naye, Katibu wa Umoja wa Watendaji Tanzania (UWATA) Bw. Frank Kalinga amesema, UWATA ni jukwaa na chombo cha kitaaluma, chenye maadili, weledi na uwajibikaji na kuongeza kuwa UWATA ni taasisi inayolenga kuwaunganisha Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa ili kuwajengea uwezo wa kitaaluma, kuimarisha maadili ya kiutumishi, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kuwa mshirika wa Serikali katika utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment