SERA YA TAIFA YA USIMAMIZI WA MNYORORO WA UGAVI NGUZO YA KUFIKIA DIRA 2050 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 30, 2026

SERA YA TAIFA YA USIMAMIZI WA MNYORORO WA UGAVI NGUZO YA KUFIKIA DIRA 2050

Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba, akieleza umuhimu wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi wakati akitoa mada katika Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026, linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba, akiwa na watoa mada wengine wakati wa Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026, linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) ambapo limeangazia kukuza uchumi wa viwanda na maendeleo ya Taifa.
Kaimu Kamishna wa Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) Wizara ya Fedha Bw. Bashiru Taratibu, akishiriki Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026, linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Afisa Ugavi Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bi. Beatrice Zenda, akitoa elimu ya Sera za Ununuzi wa Umma kupitia kipeperushi, kwa wadau wa Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026, linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Afisa Ugavi Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bw. Enock Maganga, akisikiliza hoja za Mzee Yusuph Rashid Mkazi wa Arusha kuhusu masuala ya ununuzi na fedha, katika banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026, linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Wadau mbalimbali wakishiriki Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026, linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Arusha)

Na Peter Haule, WF, Arusha

 

Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi imeelezwa kuwa nyenzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuwa inalenga kukuza uchumi wa viwanda kupitia ongezeko la matumizi ya bidhaa, huduma na malighafi zinazozalishwa nchini.

Hayo yalielezwa na Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bw. Alex Haraba, wakati akiwasilisha mada katika Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma 2026 lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Bw. Haraba alisema Sera hiyo itaongeza matumizi ya bidhaa za ndani kwa kupanua soko la wazalishaji na watoa huduma wa ndani, kuimarisha ushindani wa sekta binafsi, kuongeza ajira, mapato ya Serikali, uwekezaji na kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani.

"Lengo la sera ni kuweka msingi wa kisera wa usimamizi bora na utekelezaji wenye ufanisi wa shughuli za mnyororo wa ugavi ili kuimarisha utoaji wa huduma na matumizi ya rasilimali, kuimarisha soko la bidhaa, huduma na malighafi za ndani na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi pamoja na makundi maalumu ya kijamii," alisema Bw. Haraba.

Alifafanua kuwa Sera hiyo pia inalenga kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji yanayokidhi malengo ya ununuzi wa umma, kuboresha usimamizi wa ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali, kuimarisha mifumo ya upokeaji na urejeshaji wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi, pamoja na kuboresha utunzaji, uhifadhi, matumizi, usambazaji na uondoshaji wa bidhaa, vifaa na mali za Serikali.

Aidha, alisema Sera imezingatia masuala mtambuka ikiwemo hifadhi ya mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha misingi ya utawala bora katika shughuli zote za mnyororo wa ugavi.

Akizungumzia manufaa ya Sera hiyo, Bw. Haraba alisema katika eneo la upokeaji na urejeshaji wa bidhaa, Sera itahakikisha bidhaa, huduma na kazi za ujenzi zinakidhi viwango vya ubora, kupunguza hasara zinazotokana na bidhaa au huduma zisizokidhi viwango, kuongeza tija katika matumizi ya rasilimali za umma na kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Bw. Haraba alisema kabla ya kuanzishwa kwa Sera hiyo, shughuli za mnyororo wa ugavi zilikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kushindwa kupata mahitaji yanayokidhi malengo ya ununuzi wa umma, mifumo dhaifu ya ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali, changamoto katika upokeaji na urejeshaji wa bidhaa, udhibiti usioridhisha wa utunzaji na uhifadhi wa mali za Serikali, pamoja na ufanisi mdogo katika usambazaji na uondoshaji wa bidhaa na vifaa.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni kuzingatiwa kwa kiwango cha chini kwa masuala ya hifadhi ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na misingi ya utawala bora katika shughuli za mnyororo wa ugavi.

Alisisitiza kuwa utekelezaji kamili wa Sera hiyo unatarajiwa kuleta mafanikio makubwa, yakiwemo kuimarika kwa usimamizi wa mnyororo wa ugavi, kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa, huduma na malighafi za ndani, kuimarika kwa uzalishaji na ushindani wa viwanda vya ndani, kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi na makundi maalumu ya kijamii, pamoja na kuongeza ajira, mapato ya Serikali na matumizi yenye tija ya rasilimali za umma.


Kabla ya mwaka 2025 shughuli za ununuzi zilikuwa zikitekelezwa bila kuwepo mfumo jumuishi wa kisera unaounganisha shughuli zote za mnyororo wa ugavi, hali iliyochochea Serikali kuandaa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ili kuziba pengo hilo.

No comments:

Post a Comment