WAZIRI MKUU AZINDUA SHULE YA MSINGI KASOMA, AIPONGEZA MUSOMA VIJIJINI KWA USIMAMIZI WA MIRADI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, July 4, 2026

WAZIRI MKUU AZINDUA SHULE YA MSINGI KASOMA, AIPONGEZA MUSOMA VIJIJINI KWA USIMAMIZI WA MIRADI


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameizindua Shule ya Msingi Kasoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, mkoani Mara na kuipongeza halmashauri hiyo kwa kusimamia miradi ya maendeleo kwa kuzingatia thamani ya fedha pamoja na kuendelea kuboresha huduma za elimu kwa wananchi.

Akizungumza baada ya kuzindua shule hiyo leo (Jumamosi, Julai 4, 2026), Dkt. Mwigulu alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata fursa ya kusoma katika mazingira bora na karibu na makazi yao.

"Nimeona usimamizi mzuri wa miradi unaozingatia thamani ya fedha. Hicho ndicho ambacho Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekikusudia kiwafikie wananchi. Hongereni sana," alisema Dkt. Mwigulu.

Waziri Mkuu alisema Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imeanza mapema kutekeleza mwelekeo wa Serikali wa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya sekondari, hatua ambayo itawezesha utekelezaji wa sera ya elimu ya lazima kwa miaka 10 kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne.

"Tulipanga ifikapo mwaka 2028 tuanze utekelezaji wa mfumo huu, lakini ninyi tayari mmeanza. Hongereni sana kwa hatua hiyo," alisema.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, alisema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya elimu umeiwezesha wilaya hiyo kuendelea kupanua miundombinu ya shule ili kuendana na sera ya elimu ya lazima kwa miaka 10. Alisema jimbo hilo lina shule za msingi 120, linaendelea kujenga shule nne mpya na tayari lina shule za sekondari 33 katika kata 21, huku lengo likiwa ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya sekondari pamoja na kuongeza idadi ya shule za sekondari za juu (High Schools).

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Msongela Palela, alisema mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Kasoma ulipokea shilingi milioni 330.7 kutoka Serikali Kuu kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST). Aidha, halmashauri ilichangia shilingi milioni 5.4 kwa ajili ya ununuzi wa madawati 90, huku wananchi wa Kijiji cha Kaboni wakichangia nguvu kazi yenye thamani ya shilingi 800,000.

Alisema mradi huo umejumuisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya elimu ya awali, madarasa sita ya shule ya msingi, jengo la utawala pamoja na vyoo.

Aidha, umeondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita nne kufuata masomo, umekiwezesha Kijiji cha Kaboni kupata shule yake ya kwanza ya msingi na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

No comments:

Post a Comment