Ikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa muhula mpya wa masomo, wanafunzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Fahari Elite iliyopo Mvuti, jijini Dar es Salaam, wamepata fursa ya kujifunza kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na kukabidhiwa madaftari yenye ujumbe wa elimu hiyo mara walipotembelea banda la Wizara ya Nishati katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Wanafunzi hao, wakiongozwa na Mwalimu wao, Furaha Kyando, walipokelewa katika banda hilo na kupata elimu kuhusu maana ya nishati safi ya kupikia, aina zake na faida zake kutoka kwa Mhandisi Amina Almas.
Akizungumza na wanafunzi hao Mhandisi Amina aliwaeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanachangia kulinda afya, kuhifadhi mazingira na kuokoa muda unaotumika kutafuta nishati ambazo si safi kama vile kuni.
Madaftari waliyokabidhiwa wanafunzi hao yenye jumbe mbalimbali kuhusu nishati safi ya kupikia yatawasaidia kuendelea kujifunza na kueneza elimu hiyo shuleni, nyumbani na katika jamii.
Wanafunzi kutoka Fahari Elite ni sehemu ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali wanaotembelea banda la Wizara ya Nishati katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) na kupata madaftari yenye jumbe muhimu kama vile maana ya nishati safi ya kupikia, sifa zake, aina zake na faida zake zinazolenga kuwasaidia watoto kujifunza kwa urahisi na kuendelea kueneza elimu hiyo shuleni, nyumbani na jamii kwa ujumla.




No comments:
Post a Comment