WAZIRI NDEJEMBI ATOA ONYO KWA MKANDARASI ANAYETEKELEZA MRADI WA SONGEA–TUNDURU–MASASI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 22, 2026

WAZIRI NDEJEMBI ATOA ONYO KWA MKANDARASI ANAYETEKELEZA MRADI WA SONGEA–TUNDURU–MASASI



Na Mwandishi Wetu - Tunduru, Ruvuma


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameonesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Masasi kupitia Tunduru na kuagiza mkandarasi kuongeza juhudi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo leo Julai 22, 2026, Mhe. Ndejembi amesema Serikali haitakuwa tayari kuona miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya wananchi ikicheleweshwa bila sababu za msingi.

Amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi muhimu ya Sekta ya Nishati inayopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na mchango wake katika kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Kusini.

“Maendeleo ya mradi huu hayaridhishi ukilinganisha na muda uliopita tangu utekelezaji wake uanze. Serikali inatarajia kuona kasi kubwa zaidi ya utekelezaji katika kipindi kilichobaki. Nimemuagiza Katibu Mkuu kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo haya na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa iwapo hakutakuwa na maboresho yanayoonekana,” amesema Mhe. Ndejembi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Boniface Magiri, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, amesema Mkoa utaendelea kushirikiana na Serikali Kuu katika kufuatilia utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati.

Naye Mhe. Sikudhani Chikambo kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Ruvuma, viongozi hao wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya umeme ambayo itachochea ukuaji wa uchumi, uwekezaji na kuboresha huduma za kijamii katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania.

Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea kupitia Tunduru hadi Masasi unatekelezwa na Mkandarasi Kalpataru Power kutoka India. Mradi huo unatarajiwa kuiunganisha Mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye Gridi ya Taifa pamoja na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Tunduru na maeneo jirani.






No comments:

Post a Comment