CHAMA CHA WAZEE NGUZO YA MALEZI, UPATANISHI, UTUNZAJI MAADILI YA KIJAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 29, 2026

CHAMA CHA WAZEE NGUZO YA MALEZI, UPATANISHI, UTUNZAJI MAADILI YA KIJAMII


Na WMJJWM - DODOMA


Serikali imewataka viongozi wa Chama cha Wazee Wanaume Tanzania (CCWWT) kuhakikisha chama hicho kinakuwa chombo muhimu cha malezi, upatanishi na utunzaji wa mila, desturi na maadili ya jamii

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, katika Mkutano Chama cha Wazee Wanaume Tanzania (CCWWT) jijini Dodoma Agosti 29, 2026.

Profesa Shemdoe amesema wazee ni tunu na hazina ya Taifa kutokana na mchango wao katika malezi, makuzi na ujenzi wa jamii hivyo wana jukumu la kurithisha Hekima zao kwa Jamii.

Ameongeza pia, wazee wana nafasi kubwa ya ushauri Malezi na upatanishi wa migogoro katika jamii, hivyo wanapaswa kuwaunganisha wazee na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo. 

Aidha, Shemdoe amebainisha kwamba, Serikali inaendelea kutunza wazee ambapo jumla ya wazee 229 wapo katika makazi 13 ya wazee yanayomilikiwa na Serikali, pamoja na kutoa huduma za msaada wa kisheria kupitia Mama Samia Legal Aid kwa lengo la kulinda haki zao, ikiwemo haki ya kumiliki mali.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Maryprisca Mahundi amewahamasisha wazee kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali ikiwemo mikopo inayoratibiwa na Wizara hiyo kupitia Benki ya NMB ili waweze kupata mikopo inatakayowasaidia kuendesha miradi ya maendeleo na kuongeza kipato chao.

Mahundi ametoa wito kwa kila mwanachi kuhakikisha anatimiza wajibu wake wa kulea watoto ili wanapokuwa watu wazima waweze kuishi maisha ya uzee yenye maadili na ustawi. 


Katibu wa Chama hicho Flavian Lubuva amesema lengo la chama ni kuwaunganisha na kuwawezesha wazee kushiriki katika miradi ya maendeleo ili kujiongezea kipato na kuboresha maisha yao. 

Ametaja baadhi ya miradi inayotekelezwa na chama hicho ni pamoja na ufugaji wa nyuki mkoani Arusha, kilimo cha zabibu jijini Dodoma pamoja na uvunaji wa nyasi, ambao unalenga kutunza mazingira.

No comments:

Post a Comment