REMEMBER THE CHILDREN YAJENGA NYUMBA SABA, KUTOA MAKAZI SALAMA KWA WATOTO 126 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 29, 2026

REMEMBER THE CHILDREN YAJENGA NYUMBA SABA, KUTOA MAKAZI SALAMA KWA WATOTO 126


Na Mwandishi Wetu Tabora


Shirika la Remember the Children (RTC) limefanikiwa kujenga nyumba saba za makazi zenye uwezo wa kuhudumia watoto 126, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanapata makazi salama, malezi bora, elimu na fursa za kujenga maisha yao ya baadaye.

Hayo yamebainika wakati wa uzinduzi wa nyumba saba (7) zilizopo katika Kijiji cha Watoto kilichopo Manispaa ya Tabora mkoani Tabora kinachosimamiwa na Shirika hilo.

Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha mafanikio ya Shirika hilo, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao amesema mafanikio yaliyofikiwa na Shirika hilo ni mfano mzuri wa namna Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanavyoweza kushirikiana na Serikali, jamii na wadau mbalimbali katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili watoto.

Amesema Shirika hilo lilisajiliwa na kuanza shughuli zake nchini Tanzania mwaka 2021, likiwa na dhamira ya kuwalea na kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia mazingira salama, elimu, malezi na fursa za kujenga maisha bora ya baadaye.

“Kwa mimi ni heshima kubwa na furaha kushuhudia hatua hii iliyofikiwa. Leo ni siku yenye umuhimu mkubwa si kwetu pekee, bali pia kwa watoto na vijana ambao wamekuwa wakinufaika na huduma zinazotolewa na taasisi hii.” amesema Vickness.

Vickness ameongeza pia kwamba, nyumba hizo saba (7) hazipaswi kutazamwa kama majengo pekee, bali kama nyumba za matumaini, upendo, usalama na utu zinazowapa watoto fursa ya kukua katika mazingira yanayofanana na familia kwani mtoto hahitaji paa pekee la kumkinga, bali anahitaji upendo, malezi, usalama na mtu wa kumtia moyo na kumwambia kuwa ana thamani, uwezo na nafasi katika jamii.

Mbali na ujenzi wa makazi, shirika hilo pia limepongezwa kwa uwekezaji katika sekta ya elimu kupitia shule yake ya Intenal Pre and Primary School, inayotoa elimu kwa watoto takribani 712 wanaolelewa katika taasisi hiyo pamoja na watoto kutoka jamii inayozunguka.

Aidha amelipongeza Shirika hilo kwa uwekezaji uliofanywa katika shughuli za ufugaji wa ng'ombe wa maziwa mradi ambao unasaidia familia zinazolelewa katika taasisi hiyo kupata maziwa kwa matumizi yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Remember the Children (RTC) John Hezron amesema kila jengo linaloonekana katika eneo hilo ni matokeo ya watu na taasisi mbalimbali walioamini katika maono ya kuwapatia watoto mazingira bora ya kuishi na kukua.

Amewaomba wadau na Serikali kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanapata huduma muhimu zikiwemo makazi, elimu, afya, malezi, ulinzi na fursa za kujitegemea.


No comments:

Post a Comment