DIB YAANZA KULIPA ASILIMIA 15 ILIYOSALIA KWA WATEJA WA FBME BANK - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, August 3, 2026

DIB YAANZA KULIPA ASILIMIA 15 ILIYOSALIA KWA WATEJA WA FBME BANK


Na Shua OKULY BLOG, Morogoro


Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imeanza mchakato wa kulipa asilimia 15 ya mwisho ya fidia ya ufilisi kwa wateja wa Tanzania waliokuwa na amana katika iliyokuwa FBME Bank Limited baada ya kukusanya kiasi kinachotosheleza malipo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Bima ya amana Isack Kihwili Julai 31, 2026 mkoani Morogoro amesema kuwa, DIB ilifanya kikao cha Kamati ya Wadai Julai 29, 2026 ili kuidhinisha malipo hayo, na baada ya kupata idhini ilianza mchakato wa malipo kwa wateja husika.

Aidha kukamilika kwa malipo hayo kutawafanya wateja wa Tanzania walioweka fedha zao katika benki hiyo kulipwa asilimia 100 ya fedha zao. 

Kihwili amebainisha kuwa, FBME Bank Limited ilifungwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Mei 8, 2017 na kuwekwa chini ya ufilisi, baada ya kuthibitika kufanya vitendo vilivyokiuka masharti ya leseni ya uendeshaji wa biashara ya kibenki, kufuatia hatua hiyo, BOT iliiteua DIB kuwa mfilisi kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006. 

“Wateja wa FBME waliokuwa na amana zaidi ya shilingi milioni 1.5 walikuwa 2,280, wakiwemo wateja 1,414 wa Tanzania waliokuwa wakidai jumla ya shilingi milioni 35,233.95 na wateja 866 wa kimataifa waliokuwa na akaunti Tanzania wakidai jumla ya shilingi milioni 308,216.62”. Alisema Kihwili

Alisema hadi kufikia Juni 30, 2026, wateja wa Tanzania walikuwa wamelipwa asilimia 85 ya amana zao kupitia awamu tatu za malipo. 

Jumla ya wateja 986 kati ya 1,414 walikuwa wamelipwa fidia ya ufilisi ya asilimia 85 yenye thamani ya shilingi milioni 26,021.09 kati ya shilingi milioni 29,928.23, huku wateja 428 wakiwa hawajalipwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kutowasilisha madai yao. 

Katika hatua nyingine Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Amana Isack Kihwili alisema, baada ya kukamilisha malipo kwa wateja wa Tanzania, itaendelea kushirikiana na mfilisi wa tawi la Cyprus kukusanya mali ili kuwalipa wateja wa kimataifa, wateja wa tawi la Cyprus na baadaye wadai wengine kwa mujibu wa sheria. 

Hata hivyo, Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imewashukuru wateja wa FBME kwa uvumilivu wao na kuishukuru Serikali kwa ushirikiano, ushauri na miongozo iliyowezesha kufikia hatua hiyo ya ufilisi.

Imewashauri wananchi kuendelea kuweka amana zao katika benki na taasisi za fedha zenye leseni ya BOT kwa kuwa zinakingwa na bima ya amana kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment