Na Shua Ndereka, OKULY BLOG, Morogoro
Serikali mkoani Morogoro imeshuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa mradi wa kunyanyua tuta la Bwawa la Mindu kati ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) na kampuni ya Sinohydro ya China.
Mradi huo utagharimu shilingi bilioni 33 na unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ufaransa (AFD).
Akizungumza mara baada ya hafla ya utiaji saini, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema kampuni ya Sinohydro imeibuka mshindi wa zabuni ya kutekeleza mradi huo, ikieleza kuwa kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa baada ya kushiriki katika ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kidunda.
Malima amesema serikali imejipanga kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Morogoro.
Aidha, amekemea vitendo vya uharibifu wa mazingira katika eneo la hifadhi ya Bwawa la Mindu, akisisitiza kuwa shughuli zote zinazohatarisha vyanzo vya maji zinapaswa kusitishwa mara moja.
Amesema wananchi watakaopisha eneo la hifadhi ya bwawa watalipwa fidia zao kwa awamu, huku serikali ikitarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 9.7 kwa ajili ya zoezi hilo.
Pia ameielekeza Ofisi ya Madini Mkoa wa Morogoro kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini ndani na maeneo yanayozunguka Bwawa la Mindu zinasitishwa ili kulinda mazingira na kuhifadhi chanzo hicho muhimu cha maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA, CPA Sais Kyejo, amesema mradi huo utahusisha kunyanyua tuta la bwawa kwa urefu wa mita 2.5, hatua itakayoongeza uwezo wa bwawa kuhifadhi maji kutoka lita za ujazo bilioni 12.62 hadi zaidi ya lita za ujazo bilioni 22.
“Ongezeko hilo litasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro, huku mradi ukitarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 18 kwa mujibu wa mkataba”. Amesema CPA Kyejo
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya MORUWASA, Profesa Moses Warioba, amesema mamlaka hiyo itaendelea kuboresha huduma ya maji ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na kasi ya ukuaji wa idadi ya watu na shughuli za kijamii na kiuchumi mkoani Morogoro.
Profesa Warioba amesema upanuzi wa miundombinu ya maji ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika, huku MORUWASA ikiendelea kuweka mikakati endelevu ya kuimarisha huduma hiyo kwa maendeleo ya mkoa.





No comments:
Post a Comment