DKT. MWIGULU: TUBORESHE VIWANGO KWENYE BIDHAA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 1, 2026

DKT. MWIGULU: TUBORESHE VIWANGO KWENYE BIDHAA


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa wito kwa wazalishiaji mbalimbali nchini waboreshe bidhaa zao ili zimudu ushindani wa kimataifa na ziweze kushindana kila siku na siyo wakati wa maonesho tu.

“Bidhaa ambazo tuko nazo zisiwe kwa ajili ya maonesho, bali ndiyo iwe standard ya bidhaa zetu katika maisha yetu. Tukishafikia hatua hiyo, tutakuwa tumetatua mambo mengi kwa mpigo ikiwemo kujihakikishia kwamba bidhaa zetu zinapata soko, ni lazima tuendelee kuoanisha uzalishaji na vigezo vya kimataifa vya masoko,” amesema.

Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumamosi, Agosti Mosi, 2026) wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria ufunguzi wa Maonesho ya 33 ya Kitaifa ya Wakulima (Nanenane), yaliyofunguliwa rasmi katika Viwanja vya Dkt. John John S. Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.

Amesema kufanya hivyo kutawezesha bidhaa zinazozalishwa kupata masoko popote duniani kutokana na ubora utakaokuwa nazo. “Tutengeneze bidhaa zetu za kila siku kama vile za kwenda kwenye maonesho. Katika maeneo mengi, tatizo siyo soko bali ni viwango vinavyoweza kumsukuma mnunuzi kutamani kununua bidhaa husika. Tukiboresha viwango, bidhaa zitanunuliwa na kwa njia hiyo tutaongeza uzalishaji na hivyo kupata masoko na kuongeza uchumi wa mtu mmoja moja,” amesititiza.

Akielezea kuhusu utoshelevu wa chakula nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa nchi ina utoshelevu kwa asilimia 130 na imeongeza mauzo nje ya nchi kwa asilimia 77 na kuwa moja ya chanzo cha uhakika cha fedha za kigeni.

“Haya ni mabadiliko yanayochangiwa na hatua za serikali ya awamu ya sita kwa kuweka mazingira wezeshi na uwekezaji wenye tija kwenye mnyororo mzima wa sekta ya kilimo. Tangu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoingia madarakani, wakulima wamewezeshwa ruzuku ya pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea, zaidi ya tani 700,000 yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.4,” amesema.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea mabanda mbalimbali ya maonesho na kupata maelezo kutoka kwa wajasiriamali wanaoshiriki maonesho hayo ambapo aliipongeza Benki ya NMB kwa kuendelea kuboresha huduma za kifedha na kuzisogeza karibu na wananchi hasa wakazi wa vijijini, vijana na wanawake.

Amesema amefurahishwa na jitihada za benki hiyo za kuwafikia wananchi kupitia huduma za kibenki zinazotolewa kwa kutumia magari maalumu pamoja na kuwafuata wafanyabiashara katika masoko na minada mbalimbali nchini.

“Hatua hizi zinaendana na kiu ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuona Watanzania wengi wanapata huduma za uchumi jumuishi wa kifedha (financial inclusion) na hii itasaidia nchi kuondoka kwenye cash economy, itafanya tufike mahali mtu popote alipo ana fedha yake, na hata akitaka mahitaji fedha anayo,” amesema.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha mazingira ya sekta ya fedha, ikiwemo kupunguza gharama za miamala ya kifedha ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma bora za kibenki na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya uchumi.

Akitoa maelezo mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Idara ya Huduma za Serikali wa Benki ya NMB, Bibi Vicky Bishubo, alisema benki hiyo imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia mpango wa huduma za benki vijijini unaotumia magari maalumu ya huduma za kibenki (mobile branch operations) yanayofika katika vijiji mbalimbali nchini kutoa huduma za kifedha, elimu ya fedha pamoja na mikopo kwa wananchi hususan wanawake na vijana wajasiriamali.

Bibi Bishubo alisema pia Benki ya NMB inaendelea kushirikiana na Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya masuala ya vijana katika utekelezaji wa mpango wa mikopo wa sh. bilioni 200 ulioanzishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi. Alisema benki hiyo imeweka mazingira rafiki na kupunguza vikwazo vinavyoweza kuwazuia vijana kunufaika na mikopo hiyo.

Aidha, alisema benki hiyo inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu ya juu, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma kuandaa programu na mitaala inayolenga kuwaandaa vijana katika matumizi ya huduma za fedha za kidijitali na kuongeza uelewa wao kuhusu sekta ya fedha.

Maonesho hayo ya 33 ya Nanenane yenye hadhi ya Kitaifa na Kimataifa, yanaendeshwa kwa lengo la kukuza uchumi, kuongeza matumizi ya teknolojia bora na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

No comments:

Post a Comment