
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amewataka wafanyakazi nchini kufahamu na kufuatilia haki na stahiki zao za msingi wakati wote wa ajira, huku akisisitiza umuhimu wa kutunza nyaraka zinazoweza kutumika kama ushahidi katika kudai haki zao.
Dkt. Homera amesema wafanyakazi wanapaswa kutunza mikataba na barua za ajira, kumbukumbu za mishahara na malipo, barua za uhamisho pamoja na mawasiliano muhimu kati yao na waajiri, kwa kuwa nyaraka hizo ni sehemu muhimu ya ushahidi pale yanapotokea madai au migogoro ya ajira.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 24,2026, jijini Dodoma,katika Programu ya "SEMA NA WAZIRI" Waziri Homera amesema wafanyakazi wanaohamishwa au kutumwa vituo vipya vya kazi wanapaswa kuhifadhi nyaraka na risiti zote zinazohusiana na uhamisho na safari, ikiwemo gharama za usafiri, usafirishaji wa mizigo na fedha za kujikimu.
“Ni muhimu mfanyakazi kuwa na nyaraka na ushahidi wa stahiki zake. Hii inasaidia sana pale anapohitaji kufuatilia haki yake mbele ya mamlaka husika,” amesema Dkt. Homera.
Aidha, amesema wafanyakazi hawapaswi kusubiri hadi wanapostaafu ndipo waanze kufuatilia michango yao ya hifadhi ya jamii, bali wanapaswa kufanya ufuatiliaji mara kwa mara ili kubaini kama michango yao inaingizwa kwa usahihi.
Amesema wafanyakazi wanapaswa kuhifadhi kumbukumbu za makato ya mishahara na taarifa za michango yao na kuwasiliana na mfuko husika mara wanapobaini tofauti au changamoto katika taarifa hizo.
Kuhusu wafanyakazi wanaokumbana na kusitishwa kwa ajira, Dkt. Homera amewataka kusoma kwa makini barua za kusitishwa ajira, kutunza mikataba, nyaraka zote walizopewa na mwajiri pamoja na taarifa za malipo.
Amesema pale mfanyakazi anapoona haki zake hazijatekelezwa, anapaswa kutafuta ushauri wa kisheria na kufuata taratibu zilizowekwa badala ya kupuuza suala hilo.
Dkt. Homera pia amesisitiza kuwa migogoro ya ajira ina mamlaka na taratibu zake, hivyo wafanyakazi wanapaswa kufahamu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kulingana na aina ya mgogoro unaowakabili.
Amesema ni muhimu wafanyakazi kufahamu muda wa kufungua mashauri, kukata rufaa pamoja na kufuatilia hatua ambayo shauri limefikia katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) au mahakamani.
Kwa mujibu wa Waziri Homera, elimu hiyo imetolewa kupitia programu ya mawasiliano ya “Sema na Waziri” pamoja na kampeni ya msaada wa kisheria, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na namna ya kuzidai kwa kufuata sheria na taratibu.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuwa na ushahidi wa kutosha wanapofuatilia madai yao, kwa kuwa nyaraka na kumbukumbu sahihi husaidia mamlaka husika kuchunguza madai na kurahisisha upatikanaji wa haki.


No comments:
Post a Comment