WAZIRI MKUU ATAKA UBUNIFU UPELEKWE SOKONI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, August 24, 2026

WAZIRI MKUU ATAKA UBUNIFU UPELEKWE SOKONI

Wziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi zake kuhakikisha bunifu zinazozalishwa na Watanzania haziishii kuonyeshwa kwenye maonesho, bali zinaendelezwa, zinalindwa na kupelekwa sokoni ili zitoe suluhisho kwa changamoto mbalimbali na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.


Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo, Jumatatu, Agosti 24, 2026, jijini Tanga wakati akihitimisha Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, akisisitiza umuhimu wa kujenga mfumo unaowawezesha wabunifu kubadilisha mawazo yao kuwa bidhaa na huduma zenye tija.


Amesema Tanzania ina wabunifu wenye uwezo mkubwa katika maeneo mbalimbali, hivyo hatua inayohitajika sasa ni kuhakikisha ubunifu huo unavuka hatua ya kuoneshwa kwenye maonesho na kufikia hatua ya kutumika, kuzalishwa kwa wingi na kuuzwa sokoni.


“Ni lazima tuvuke kwenye maonesho, twende kwenye uhalisia wa maisha kwamba hivi vitu ambavyo tunavionyesha kwenye maadhimisho kama haya sasa viende kwenye utaratibu wa kila siku wa maisha, tuvitengeneze vya kutosha, vitumike na viingie sokoni,” amesema Dkt. Mwigulu.


Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sayansi, ujuzi na ubunifu kwa lengo la kuyageuza maeneo hayo kuwa nguzo muhimu za uchumi wa Taifa na kuchochea maendeleo kupitia matumizi ya tafiti na teknolojia.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema maonesho hayo yanaakisi jitihada za Serikali katika kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha elimu inayounganisha nadharia na vitendo, ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi wa kujiajiri na kuingia kwa ufanisi katika soko la ajira.


Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Caroline Nombo amesema jumla ya taasisi 91 za umma na binafsi zimeshiriki katika maadhimisho hayo, ambayo yamehusisha maonesho ya elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu, mashindano ya kitaifa ya ujuzi na ubunifu pamoja na makongamano yaliyolenga kujadili mchango wa elimu, ujuzi na teknolojia katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe Husna Sekiboko amesema Bunge litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuendeleza elimu, ujuzi na ubunifu kupitia bajeti, sera na miongozo inayolenga kuwawezesha watafiti na wabunifu wa ndani kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani amesema uwekezaji wa Serikali katika sekta ya elimu umeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia mkoani humo na kuchochea mafanikio ya wanafunzi, huku akipongeza maonesho hayo kwa kuibua na kuonesha uwezo mkubwa wa Watanzania katika sayansi, teknolojia na ubunifu.


Kaulimbiu ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu mwaka 2026 ni “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”





No comments:

Post a Comment