Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Zanzibar, Bi. Mariam Saleh Tuzo ya shukran kutokana na mchango wa Mfuko huo kuwa miongoni mwa Taasisi zilizofanikisha kufanyika kwa Kongamano hilo ambalo ni sehemu ya Tamasha la 10 la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar usiku wa kuamkia leo Agosti 12, 2026.
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Taasisi zilizopatiwa tuzo
Rais wa Zaznibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (Kushoto) na mkewe Mama Mariam Mwinyi (mwenye raba nyekundu), wakitembelea mabanda ya Maonesho baada ya kuzindua Tamasha la Kizimkazi Agosti 12, 2026

Meneja wa PSSSF Zanzibar, Bi. Mariam Saleh, akiwa na Tuzo ya shukrani baada ya kukabidhiwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kukabidhiwa
Zanzibar, Agosti 12, 2026
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameutunuku Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) tuzo ya kutambua mchango wake katika kuwezesha kufanyika kwa Mdahalo wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, uliofanyika Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, usiku wa kuamkia leo, Agosti 12, 2026.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa Meneja wa PSSSF Zanzibar, Bi. Mariam Saleh, kwa niaba ya Mfuko, ikiwa ni sehemu ya utambuzi kwa taasisi na wadau walioshiriki katika kuwezesha mdahalo huo, uliofuatiwa na Maonesho ya Picha za Tamasha la Kizimkazi.
Mdahalo huo umefanyika sambamba na Tamasha la 10 la Kizimkazi (Kizimkazi Festival 2026), linalofanyika Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, ambapo tamasha hilo limeanza rasmi leo kwa matembezi pamoja na uzinduzi uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Ushiriki wa PSSSF katika mdahalo huo unaakisi dhamira ya Mfuko ya kushirikiana na Serikali, taasisi na wadau mbalimbali katika kuunga mkono mijadala yenye umuhimu kwa jamii, mazingira na maendeleo endelevu.
Aidha, PSSSF inawakaribisha wanachama na wananchi kutembelea banda la Mfuko katika Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi yanayoanza leo, Agosti 12, 2026, kwa ajili ya kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa na Mfuko, amesema Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bi. Fatma Elhady.
Mwisho

No comments:
Post a Comment