WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imejipanga vema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa kuanza mwezi ujao hasa katika maeneo yanayopata mvua nyingi.
Ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma, leo (Alhamisi, Agosti 27, 2026) wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Mjini, Mha. Johnston Mutasingwa, kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa miundombinu ya barabara na makazi ya wananchi kulingana na tahadhari ambayo imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) juu ya uwepo wa El-Nino yenye nguvu.
“Ni kweli tumepata tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini juu ya uwepo wa mvua kubwa za El-Nino na hasa kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako mvua hizo zinatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Septemba ama Oktoba mwanzoni. Serikali imejipanga kwa kuandaa mifereji katika maeneo hayo ili kuondoa uwezekano wa maji kurundikana.”
Waziri Mkuu amesema Serikali imeelekeza TANROADS na TARURA zifanye ukaguzi wa barabara, madaraja, makalavati na mifereji ya maji ili kubaini mapema maeneo korofi yanayoweza kuathiriwa ili kuhakikisha wananchi hawakosi miundombinu kutokana na mafuriko.
“Bunge lako tukufu lilielekeza fedha za mifuko ya barabara ziwe zinakwenda moja kwa moja kwenye mifuko ya barabara badala ya Serikali kuu. Nimpongeze Waziri wa Fedha pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuanza kutekeleza uamuzi huo ambapo kwa mwezi zaidi ya sh. bilioni 320 zinaenda moja kwa moja kweye mifuko na kuiwezesha kukabiliana na mambo kama haya,” amesema.
Amewataka Watanzania wachukue tahadhari kwa kila mmoja kufanya tathmini ya mahali wanapoishi kwa kuangalia mazingira ya mahali walipo kwani wanajua ni wapi maji huwa yanapita au yanatuama. “Tuendelee kuchukua hizo tahadhari ili maafa yasitokee ilhali tumeshatahadharishwa,” amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amempongeza Deogratius John Ndejembi kwa kuaminiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kamati Kuu ya CCM na Halmashauri Kuu ya CCM na kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Mwigulu ameitumia nafasi hiyo pia kumpongeza Rais Samia kwa kuwa na jicho la kipekee hadi akamuona Mheshimiwa Ndejembi. Amesema kiongozi huyo anazo sifa zinazomfanya astahili kupewa dhamana hiyo kubwa ya kitaifa.
“Mheshimiwa Naibu Spika, Deogratius Ndejembi ni kiongozi mahiri sana, ni kiongozi makini, ni kiongozi mchapakazi anayefanya kazi bila kuchoka ili Watanzania waweze kupata manufaa. Ndejembi pia ana sifa za unyenyekevu na upole, ni mtu rahimu asiye na hiana ndani yake,” amesema.
Waziri Mkuu amemhakikishia Mheshimiwa Ndejembi kuwa yeye pamoja na mawaziri wenzake wako tayari kushirikiana naye wakati akitekeleza majukumu yake mapya katika kuijenga Tanzania.


No comments:
Post a Comment