Na Shua Ndereka, OKULY BLOG, Morogoro
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kuendelea kuimarisha uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya michezo shuleni kupitia uboreshaji wa miundombinu, kuwajengea uwezo walimu wa michezo na kuimarisha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ili kuibua vipaji vitakavyoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI), Dkt. Festo Ndugage, katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, wakati akifunga rasmi Mashindano ya Michezo ya Shule za Msingi na Sekondari kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) 2026, yaliyofanyika kwa siku 10 mkoani humo yakihusisha washiriki kutoka nchi tano ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Dkt. Ndugage alisema katika kipindi chote cha mashindano hayo, Mkoa wa Morogoro umegeuka kuwa kitovu cha vipaji, nidhamu na urafiki, huku akisisitiza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga amani, kuimarisha uchumi na kuzalisha ajira kupitia sekta ya michezo.
Aliwapongeza wanafunzi wote walioshiriki mashindano hayo pamoja na washindi katika michezo mbalimbali, akieleza kuwa ushindani uliooneshwa, hususan katika fainali iliyozikutanisha Tanzania na Uganda, umeonesha kiwango kikubwa cha vipaji vinavyopaswa kuendelezwa.
"Endeleeni kufanya mazoezi kwa bidii, waheshimuni walimu wenu, dumisheni undugu na uzalendo na FEASSA 2026 isiwe mwisho wa safari yenu, bali iwe mwanzo wa kufungua milango ya kushiriki mashindano makubwa zaidi" alisema Dkt. Ndugage.
Pia Dkt. Ndugage alishuhudia fainali ya mpira wa miguu kati ya timu ya Morogoro Sekondari ya Tanzania na St. Mary's ya Uganda, ambapo Uganda iliibuka mshindi kwa mabao 2-1 dhidi ya Morogoro Sekondari, ushindi uliowapa taji lao la 17 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.
Aidha, aliuomba uongozi wa FEASSA kuanza kutumia teknolojia ya mfumo wa marudio ya matukio ya mchezo (video replay), kwa kuweka runinga kubwa viwanjani ili kusaidia maamuzi ya waamuzi, pale panapotokea utata kwani hatua hiyo itawajengea uzoefu wanamichezo wanaojiandaa kushiriki mashindano ya kimataifa.
Katika hatua nyingine Dkt. Ndugage aliwapongeza viongozi wa Mkoa wa Morogoro kwa kufanikisha maandalizi ya mashindano hayo kwa amani na utulivu, akisema wageni kutoka nchi zilizoshiriki wameonesha kuridhishwa na maandalizi, huduma za malazi pamoja na miundombinu ya michezo iliyotumika.
"Ndugu washiriki na wanamichezo, tunapofunga mashindano haya tusifunge roho ya umoja na undugu tulioujenga, tuipeleke roho hii katika shule zetu na jamii zetu ili kujenga Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye amani, ustawi na maendeleo ya kweli”. Alisema Dkt. Ndugage
Awali, Rais wa Shirikisho la FEASSA, Justice Mugisha, aliishukuru Serikali ya Tanzania na uongozi wa Mkoa wa Morogoro ukiongozwa na Mkuu wa mkoa Adam Malima kwa maandalizi mazuri, yaliyowezesha mashindano hayo kufanyika kwa mafanikio makubwa, huku akiwapongeza washindi wote na kuwashukuru wadhamini kwa mchango wao uliofanikisha kufanyika kwa mashindano hayo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Atupele Mwambene, alisema mashindano ya FEASSA ni jukwaa muhimu la kuwajengea wanafunzi nidhamu, afya njema na uwezo wa kushindana kimataifa, huku akiwapongeza walimu na walezi wote kwa mchango wao katika kuwaandaa wanamichezo.
Katika mashindano hayo yaliyoanza Agosti 12, Tanzania iliendelea kuwa bingwa kwa mara ya tatu mfululizo katika michezo ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu, huku upande wa shule za msingi na sekondari, Kenya iliibuka bingwa wa jumla, Rwanda ikawa mshindi wa pili katika shule za msingi, Uganda ikashika nafasi ya pili kwa shule za sekondari, huku Tanzania ikimaliza katika nafasi ya tatu kwa shule za msingi na sekondari.
Naye Kiongozi wa Timu ya Kenya, Boniphace Mwakio, alisema wanafurahia ushindi huo wa pili mfululizo tangu mwaka 2025, akieleza kuwa umetokana na maandalizi ya mapema ikiwa watakaporejea Kenya wataendelea kujipanga zaidi, hususan katika mpira wa miguu wa wasichana, kuelekea mashindano ya FEASSA yajayo.
Katika hafla hiyo ya kufunga mashindano Agosti 22, 2026, bendera ya FEASSA ilikabidhiwa kutoka Tanzania, mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2026, kwenda Rwanda, ambayo itakuwa mwenyeji wa Mashindano ya FEASSA mwaka 2027.







No comments:
Post a Comment