TARURA SINGIDA YAWAJENGEA UELEWA WATUMISHI WAKE KUHUSU UTEKELEZAJI WA CBRM - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 22, 2026

TARURA SINGIDA YAWAJENGEA UELEWA WATUMISHI WAKE KUHUSU UTEKELEZAJI WA CBRM


Na Mwandishi Wetu - Singida


Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Singida umeendesha mafunzo kwa watumishi wake ambao hawakupata fursa ya kushiriki katika mafunzo yaliyotolewa awali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Matengenezo ya kawaida ya Barabara kwa kutumia vikundi vya kijamii (CBRM).

Mafunzo hayo mefanyika mwisho wa wiki ambayo yamewahusisha Maafisa Hesabu, Ununuzi, Sheria, Wakaguzi wa Ndani, Wachumi, Mazingira, Ustawi wa Jamii pamoja na Wahandisi kutoka ofisi ya Meneja wa Mkoa. 

Akitoa mafunzo hayo Mshauri Mwelekezi wa Mpango wa CBRM, Mhandisi Laurent Kyombo  amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na mshikamano katika ngazi zote za utekelezaji wa mradi ili kuwezesha timu kukabiliana na changamoto zozote zitakazo jitokeza  wakati wa utekelezaji wa mpango huo.

Aidha, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa watumishi kwa kuwa yanawajengea uelewa wa kujua muda uliopangwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli  mbalimbali pamoja na hatua zinazopaswa kufikiwa ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango unaanza na kumalizika kwa wakati kama ulivyopangwa.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Claver Mwinuka amesema mafunzo hayo yamelenga kufuatilia utekelezaji wa shughuli za CBRM, kukumbushana na kujadili masuala muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa mpango huo.

Mhandisi Mwinuka ameongeza kusema kwamba mafunzo hayo yataleta mwamko mpya kwa timu ya Mkoa, kwa kuwa yamewezesha kujadili masuala mbalimbali ya msingi huku changamoto zilizotokana na tofauti za uelewa zikitafutiwa ufumbuzi na watumishi kupewa mwongozo wa utekelezaji.

Naye, Mratibu wa Mradi wa CBRM Mkoa wa Singida Mhandisi Gisela Maro, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya TARURA, wananchi na wadau wengine katika kuhakikisha mpango wa CBRM unatekelezwa kwa ufanisi na kufikia matokeo yaliyokusudiwa.

Ameongeza kuwa kufanikiwa kwa mpango huo itaimarisha miundombinu ya barabara na kuboresha maisha ya wananchi kupitia fursa za ajira kwani kipato kitaongezeka.

Amesema utekelezaji wa mpango huo unalenga, miongoni mwa mambo mengine, kuimarisha miundombinu ya barabara pamoja na kuboresha maisha ya wananchi kupitia fursa za ajira na kuongeza kipato.

Mhandisi Maro ameahidi kuwa Mkoa wa Singida utaendelea kuhakikisha wadau wote wanashirikishwa na kwamba malengo yaliyowekwa kupitia mpango wa CBRM yanafikiwa kwa ufanisi na bila kikwazo.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TARURA Mkoa wa Singida katika kuhakikisha watumishi wake wanakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu majukumu, taratibu na hatua muhimu za utekelezaji wa mpango wa CBRM, ili kuuwezesha mpango huo kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment