Wizara ya Afya kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, imetoa elimu ya afya kuhusu mtindo bora wa maisha na Magonjwa Yasiyoambukiza (MYA), pamoja na kutoa huduma za uchunguzi wa afya bila malipo katika viwanja vya mpira vya Kwaraa, Manyara, wakati wa Manyara Tanzanite Marathon.
Elimu hiyo imejikita katika kampeni ya “Zijue Namba Zako”, ikiwahamasisha wananchi kufahamu hali ya afya zao kwa kufanya vipimo mbalimbali, ikiwemo uwiano wa urefu na uzito, pamoja na kujenga utamaduni wa kuchunguza afya mara kwa mara ili kubaini changamoto mapema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, Mhe. George Bajuta, amepongeza huduma na elimu hiyo, akisema imekuwa fursa muhimu kwa wananchi kupata elimu na kuchunguza afya zao bila malipo.
«“Nashukuru sana Wizara ya Afya kupitia Elimu ya Afya kwa Umma kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa kuja na programu hii bure katika Manyara Tanzanite Marathon. Nitoe wito kwa wananchi tuchunguze afya zetu,” amesema.»
Aidha, Mhe. Bajuta amepongeza programu ya “Ongea na Waziri 199”, akisema imekuwa na mchango mkubwa katika kuwafikia wananchi na kuwawezesha kupata taarifa na ushauri kuhusu masuala ya afya.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Masakta, Mhe. Thobias Gitiyanga, amesema wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara badala ya kusubiri hadi tatizo la kiafya litokee.
Naye Novat Pilot, mmoja wa wananchi waliojitokeza katika mabanda ya Wizara ya Afya na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, amepongeza elimu iliyotolewa, hususan kuhusu lishe bora, umuhimu wa kula mlo kamili na kufanya mazoezi kwa ajili ya kulinda afya.
Ikumbukwe kuwa Manyara Tanzanite Marathon inalenga kuchangia ujenzi wa jengo la kuhudumia watoto waliozaliwa kabla ya wakati (njiti), pamoja na ununuzi wa vifaa muhimu kwa ajili ya huduma hizo.
Katika mbio hizo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara imeshiriki kutoa elimu ya afya, vipeperushi pamoja na kitabu kinachohusu “Mtindo wa Maisha na Magonjwa Yasiyoambukiza”, kwa lengo la kuendelea kuhamasisha wananchi kuchukua hatua za kulinda afya zao.







No comments:
Post a Comment