Serikali yasisitiza usimamizi imara wa maji chini ya ardhi - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 7, 2026

Serikali yasisitiza usimamizi imara wa maji chini ya ardhi


Serikali imezitaka kampuni na wadau wote wanaojihusha na utafiti na uchimbaji wa maji chini ya ardhi kuzingatia utaratibu wa kuwa na nyaraka halali za sheria, leseni na kukidhi viwango vya kitaalamu ili kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo na usalama wa taifa.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akifungua Warsha ya Wadau wa Maji Chini ya Ardhi ya mwaka 2026 jijini Dodoma, amesema maji chini ya ardhi ni akiba ya kimkakati inayosaidia kuhakikisha upatikanaji wa maji safi, hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema uchimbaji holela wa visima unahatarisha ubora na uendelevu wa rasilimali hiyo, hivyo Serikali itaendelea kuimarisha ukaguzi, utoaji wa leseni na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika usimamizi wa sekta.

Amewataka wadau kushiriki kikamilifu katika kampeni ya “1575 Tupo Site Kikazi Zaidi”, inayolenga kuhakikisha vijiji vilivyosalia vinapata huduma ya uhakika ya maji kwa ushirikishwaji wa sekta binafsi.

Ameelekeza Wizara ya Maji kuboresha kanzidata ya visima, kuanzisha mfumo wa kidigitali wa utoaji wa leseni na vibali, kuimarisha mafunzo ya wataalamu pamoja na kuanzisha Umoja wa Wadau wa Maji Chini ya Ardhi ili kuimarisha weledi, uwajibikaji na ushindani wa kiwango.

Waziri Aweso amewataka washiriki wa warsha kutoa mapendekezo yatakayosaidia kulinda na kuendeleza rasilimali ya maji chini ya ardhi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri katika warsha hiyo amesisitiza uadilifu, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kutatua changamoto za maji chini ya ardhi.

 Amewahakikishia wadau wote wa maji kuwa serikali ipo pamoja nao kuhakisha changamoto wanazokutana nazo katika kutekeleza majukumu yao zinapatiwa ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment