SERIKALI YAWEKA MSISITIZO KWA VIJANA KUPATA AJIRA, KUJIAJIRI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 13, 2026

SERIKALI YAWEKA MSISITIZO KWA VIJANA KUPATA AJIRA, KUJIAJIRI




Na Boniphace John – Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amesema Serikali imeendelea kuweka msisitizo katika kuandaa mazingira yatakayowawezesha vijana kupata ajira, kujiajiri na kutumia ujuzi wao kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.


Amesema ongezeko la vijana wanaoingia katika soko la ajira limeendelea kuhitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kuongeza fursa za ajira na kuwawezesha vijana kiuchumi.


Waziri Nanauka amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika elimu, afya, miundombinu na huduma za jamii, huku sekta binafsi ikiendelea kuwa mshirika muhimu katika kuongeza ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana.


Amezitaja sekta za ujenzi, viwanda, kilimo, biashara na huduma kuwa miongoni mwa maeneo yenye uwezo mkubwa wa kutoa fursa kwa vijana, sambamba na hatua za kuwawezesha kujiajiri na kukuza ubunifu.


Amebainisha hayo Agosti 12, 2026, jijini Dodoma, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana, ambapo wadau mbalimbali walijadili fursa na changamoto zinazowakabili vijana, ikiwemo ajira, ujasiriamali, teknolojia, afya, ushiriki katika maamuzi na usawa wa fursa.


Maadhimisho hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu inayosisitiza “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana.”


Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bi. Susan Ngongi Namondo, amesema zaidi ya Mtanzania mmoja kati ya watatu ana umri wa kati ya miaka 15 na 35, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, hali ambayo imeifanya ajenda ya vijana kuwa muhimu katika mipango ya maendeleo ya Taifa.


Amesema ukosefu wa uhakika wa kiuchumi, pengo la kidijitali na mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili vijana, huku akisisitiza matumizi ya teknolojia na akili bandia katika kuwawezesha vijana kutatua changamoto za maendeleo.


Ngongi amesema vijana hawajaanza maisha katika mazingira yanayofanana, hivyo usawa wa fursa haumaanishi kuwapa wote msaada unaofanana, bali kunahitajika kutambua na kuondoa vikwazo vinavyowakabili katika mazingira yao.


Amesema vijana wanahitaji elimu bora, ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko, mitaji, teknolojia, ushauri na mitandao ili waweze kubadili mawazo yao kuwa biashara na kupata ajira zenye staha.


Amesisitiza kuwa vijana hawapaswi kusaidiwa kutumia teknolojia pekee, bali wanapaswa pia kuwezeshwa kuibuni, kuiendeleza na kuitumia kwa uwajibikaji.



No comments:

Post a Comment