SH. BILIONI 9 KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI, WANANCHI 437,200 KUNUFAIKA DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 21, 2026

SH. BILIONI 9 KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI, WANANCHI 437,200 KUNUFAIKA DODOMA



Na Okuly Julius,OKULY BLOG, DODOMA

Wananchi 437,200 wa Jiji la Dodoma na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Bahi wanatarajiwa kunufaika na mradi wa miaka mitano wenye thamani ya Sh. bilioni tisa unaolenga kuboresha huduma za maji, kupunguza upotevu wa maji na kuimarisha ufanisi wa mamlaka zinazotoa huduma hiyo.

Mradi huo unalenga pia kuboresha upatikanaji wa maji salama na ya uhakika, kuongeza ufanisi wa mifumo ya usambazaji, kurejesha uwezo wa miundombinu iliyopo, pamoja na kuimarisha uwezo wa wataalamu na taasisi zinazohusika na usimamizi wa huduma za maji.

Akizungumza Agosti 21, 2026, wilayani Bahi, mkoani Dodoma, katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa kuanzisha mfumo wa majaribio, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali ya Korea kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA).

Amesema mradi huo hautalenga kuongeza miundombinu mipya pekee, bali pia kuboresha matumizi ya miundombinu iliyopo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa ufanisi na kwa muda mrefu.

“Mradi huu utanufaisha wananchi wa Jiji la Dodoma na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Bahi. Thamani ya mradi huo haipimwi kwa kiasi cha fedha kilichowekezwa pekee, bali pia kwa manufaa yatakayopatikana kwa wananchi na uwezo wa huduma hizo kuendelea kutolewa kwa ufanisi kwa muda mrefu,” amesema.

Mhandisi Mwajuma alisema Serikali inaendelea kuweka kipaumbele katika kuongeza ufanisi wa huduma za maji na kupunguza upotevu wa maji, akieleza kuwa maji yanayozalishwa lakini hayamfikii mtumiaji au hayalipiiwi ipasavyo ni hasara kwa taasisi zinazotoa huduma na Taifa kwa ujumla.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia sera na mikakati inayolenga kuhakikisha rasilimali ya maji inatumika kwa ufanisi, huku mamlaka za maji zikiimarisha uwezo wa kutoa huduma endelevu kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, mradi huo pia utatoa fursa ya kujifunza na kupata uzoefu ambao unaweza kutumika kama mfano katika maeneo mengine nchini, hususan katika kuongeza ufanisi wa huduma na kupunguza upotevu wa maji.

Kwa upande wake, Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania, Eunju Ahn, alisema mradi huo unatarajiwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuboresha usimamizi wa maji nchini na kusaidia Wizara ya Maji, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) pamoja na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuimarisha mikakati ya kitaifa ya utunzaji wa miundombinu ya maji.

Amesema ushirikiano wa maendeleo kati ya Korea na Tanzania umefikia takribani dola milioni 875 katika kipindi cha mwaka 1987 hadi 2024, hali inayodhihirisha kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa maendeleo kati ya mataifa hayo mawili.

“Mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama, kupunguza upotevu wa maji yasiyolipiwa, pamoja na kuimarisha mifumo ya usambazaji na usimamizi wa maji,” amesema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, amesema mradi huo pia unalenga kurejesha na kuongeza ufanisi wa miundombinu iliyopo badala ya kutegemea ujenzi wa miundombinu mipya pekee.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha miundombinu iliyopo inafanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuongeza uwezo wa mamlaka hiyo kutoa huduma ya maji kwa uhakika kwa wananchi.









No comments:

Post a Comment