TANTRADE YAWATAKA WAZALISHAJI KUTUMIA FURSA ZA MASOKO YA NDANI NA NJE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, August 9, 2026

TANTRADE YAWATAKA WAZALISHAJI KUTUMIA FURSA ZA MASOKO YA NDANI NA NJE



Na Boniphace John – Dodoma

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imewataka wazalishaji wa bidhaa na watoa huduma nchini kutumia ofisi za mamlaka hiyo kupata elimu na taarifa kuhusu viwango vya ubora, gharama na mikakati bora ya biashara ili kuongeza ushindani wa bidhaa zao katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati wa kufunga Maonesho ya 33 ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Ephraim Balozi Mafuru, amesema Tanzania kwa sasa inauza bidhaa nje ya nchi zenye thamani ya takribani dola bilioni 10 za Marekani kwa mwaka.

Amesema TANTRADE inaamini kuwa Tanzania ina uwezo wa kuongeza thamani ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na kufikia zaidi ya dola bilioni 20, ikiwa wazalishaji watazingatia ubora, kuongeza thamani ya bidhaa na kuelewa mahitaji ya masoko ya kimataifa.

Mafuru amesema TANTRADE itaendelea kufanya tafiti za masoko kwa kubaini mahitaji ya walaji, kuelewa vigezo vya ubora vinavyohitajika katika masoko mbalimbali pamoja na kuchambua gharama zinazotumika katika mnyororo mzima wa thamani.

Hata hivyo, amesema kufikia lengo hilo kunahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na wadau wengine, huku wazalishaji wakitakiwa kuelewa mahitaji ya masoko ya kimataifa na kuhakikisha bidhaa zao zinafikia viwango vinavyokubalika.

“Tunataka wazalishaji kutumia TANTRADE kama kituo cha kupata taarifa za masoko, viwango vya ubora na fursa zilizopo, kwa sababu tunalenga kuona bidhaa zinazozalishwa nchini zinaingia katika masoko mengi zaidi,” amesema Mafuru.

Amesema TANTRADE itaendelea kushirikiana na wazalishaji wa ndani kuboresha ubora na ushindani wa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, hatua ambayo itasaidia kuongeza thamani ya bidhaa na kufungua masoko mapya ndani na nje ya Tanzania.

Kwa upande mwingine, Mafuru amesema Maonesho ya Nanenane yameendelea kuonyesha ongezeko la uzalishaji na biashara ya bidhaa zinazotengenezwa nchini, huku wazalishaji wakiboresha ubora wa bidhaa zao na kuanza kufikia masoko ya kimataifa.

Amesema maonesho hayo ya siku nane yamewakutanisha zaidi ya waoneshaji 1,300 kutoka katika sekta mbalimbali za uzalishaji na biashara, yakitoa fursa ya kutangaza bidhaa, kuhamasisha uwekezaji na kuwaunganisha wazalishaji na masoko.

Mafuru amesema kupitia kampeni ya “Made in Tanzania”, TANTRADE inalenga kuhakikisha bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini zinatambulika zaidi, zinafikia viwango vinavyohitajika na kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

Amesema ushiriki wa TANTRADE katika maonesho mbalimbali nchini unalenga kuwafikia wazalishaji moja kwa moja na kuwapatia taarifa kuhusu fursa za masoko, viwango vya ubora, mahitaji ya walaji pamoja na namna bora ya kuongeza thamani ya bidhaa zao.

Amesisitiza kuwa wazalishaji wanapaswa kutumia fursa hizo kujifunza, kuboresha bidhaa zao na kujenga uwezo wa kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa.

No comments:

Post a Comment