MUSOMA YATOA TENDA ZA SH. MILIONI 99 KWA MAKUNDI MAALUM, USAJILI WAVUKA LENGO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, August 9, 2026

MUSOMA YATOA TENDA ZA SH. MILIONI 99 KWA MAKUNDI MAALUM, USAJILI WAVUKA LENGO


Halmashauri ya Manispaa ya Musoma imesajili makundi maalum 157 ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, ikiwa ni zaidi ya lengo la kusajili makundi 150, huku ikitoa zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 99 kwa makundi sita.

Hayo yamebainishwa Agosti 7, 2026, wakati Mbio za Mwenge wa Uhuru zilipozuru na kukagua miradi katika Halmashauri hiyo, kisha kutembelea mabanda ya maonesho katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mwisenge.

Afisa Ununuzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Alphonce Julius, akiwa katika banda la PPRA, alimweleza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Bw. Wazo Michael Mwang’onda, kuwa pamoja na mafanikio hayo ya awali, Halmashauri imejipanga kutoa zabuni zaidi kwa makundi maalum hadi kufikia asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi, kwa mujibu wa sheria.

Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa aliipongeza Halmashauri kwa kuvuka lengo, akiitaka kuhakikisha inatoa fursa kwa wananchi waliojisajili katika makundi hayo na kuwahamasisha wengine kujisajili ili kuimarisha ustawi wa jamii kiuchumi.

“Mmefanya jambo jema kufikia lengo. Lakini sasa hakikisheni makundi haya mliyoyasajili mnayatengenezea mazingira mazuri ya kupata zabuni kupitia Mfumo wa NeST. Hii ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuona kila Mtanzania anapata fursa ya kujiinua kiuchumi kupitia zabuni hizi zinazotolewa,” amesema Mwang’onda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa, Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru umekagua na kuzindua miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 15 katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.

No comments:

Post a Comment