
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kulia), akiagana na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF), nchini Tanzania Bi. Elke Wisch, mara baada ya kikao chao kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo walijadili masuala mbalimbali katika kuboresha afya, lishe, elimu na ustawi wa watoto, na utekelezaji wa malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa kikao chake na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Elke Wisch (hayupo pichani), kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambacho kilijadili masuala mbalimbali katika kuboresha afya, lishe, elimu na ustawi wa watoto, na utekelezaji wa malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Bi. Elke Wisch, akizungumza jambo wakati wa kikao na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), ambacho kilijadili masuala mbalimbali katika kuboresha afya, lishe, elimu na ustawi wa watoto, na utekelezaji wa malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo alisema UNICEF inajivunia ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania katika kufuatilia maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan katika maeneo yanayogusa haki na ustawi wa watoto, na kwamba shirika hilo litaendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kukuza maendeleo ya rasilimali watu.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza kikao chake na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Elke Wisch, kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambacho kilijadili masuala mbalimbali katika kuboresha afya, lishe, elimu na ustawi wa watoto, na utekelezaji wa malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Elke Wisch (wa tatu kushoto), Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade (wa pili kushoto), Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule (kushoto), na maafisa wengine waandamizi wa UNICEF, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kikao chao kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambacho kilijadili masuala mbalimbali katika kuboresha afya, lishe, elimu na ustawi wa watoto, na utekelezaji wa malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)
Na. Joseph Mahumi, Dar es Salaam
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF) limeipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua kubwa zilizopigwa katika kuboresha afya, lishe, elimu na ustawi wa watoto, na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Bi. Elke Wisch, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Bi. Wisch alisema UNICEF inajivunia ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania katika kufuatilia maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan katika maeneo yanayogusa haki na ustawi wa watoto, na kwamba shirika hilo litaendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kukuza maendeleo ya rasilimali watu.
Alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, ikiwemo kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano na kupunguza kiwango cha udumavu kwa watoto.
“Tunatambua na kupongeza maendeleo haya, lakini bado kuna changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele, hasa katika siku 1,000 za mwanzo za maisha ya mtoto, elimu, lishe na maendeleo ya awali ya mtoto,” alisema Bi. Wisch.
Katika eneo la lishe, Bi. Wisch amesema Tanzania imepunguza kiwango cha udumavu kutoka takribani mtoto mmoja kati ya watoto wawili mwaka 1992 hadi mtoto mmoja kati ya watoto watatu katika miaka ya karibuni.
Aliongeza kuwa UNICEF imeendelea kushirikiana na Serikali katika kuandaa hoja za uwekezaji katika maendeleo ya awali ya mtoto na lishe, huku ikipendekeza kufanyika kwa majadiliano ya kitaifa kuhusu ufadhili wa maendeleo ya awali ya mtoto ili kuunganisha rasilimali kutoka Serikalini, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na taasisi za uhisani.
Bi. Wisch ameishukuru Serikali kwa ushirikiano katika masuala ya uwazi wa bajeti, uchambuzi wa bajeti na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha, hatua zilizochangia kuimarisha nafasi ya Tanzania katika viwango vya kimataifa vya uwazi wa bajeti.
“UNICEF itaendelea kusaidia kujenga uwezo wa Serikali katika uchambuzi na ufuatiliaji wa bajeti katika ngazi ya Taifa na Serikali za Mitaa, hususan kwa kuwa huduma nyingi zinazowahusu watoto hutolewa katika ngazi hizo” alisema Bi Wisch.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) alisema kuwa UNICEF ni mdau muhimu nchini Tanzania kwa kuwa linalenga kundi la watoto na vijana chini ya umri wa miaka 18, ambalo linafikia takribani watu milioni 30, ambalo ni sehemu muhimu ya mustakabali wa Taifa na linahitaji kupewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo.
Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, ajenda ya UNICEF nchini ina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha watoto wanapata huduma muhimu zinazowawezesha kukua katika mazingira bora, zikiwemo afya ya mama na mtoto, elimu, lishe na maendeleo ya awali ya mtoto.
Alisema uwekezaji katika watoto na vijana ni uwekezaji katika nguvu kazi ya Taifa ya baadaye, kwa kuwa kundi hilo bado halijafikia umri wa uzalishaji na hivyo linahitaji kuwezeshwa kwa huduma na mazingira bora yatakayowaandaa kuwa rasilimali watu yenye tija.
“Tunapaswa kuwekeza kwao leo kwa ajili ya kazi ya kesho, na kujenga mtaji watu ambao utakuwa msingi wa maendeleo ya Taifa, kwa kuwa mtaji watu hauishii katika elimu pekee bali unahusisha pia afya bora, lishe, malezi na ustawi wa mtoto” alisema Mhe. Balozi Omar
Mhe. Balozi Omar aliahidi kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana kwa karibu na UNICEF katika maeneo yanayohusiana na majukumu yake, akieleza kuwa masuala ya watoto, afya, elimu, lishe na ujenzi wa mtaji watu yana uhusiano wa moja kwa moja na mipango na bajeti ya Serikali.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule, na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na UNICEF.

No comments:
Post a Comment