USHETU YATOA ZABUNI ZA SH. MILIONI 90.48 KWA MAKUNDI MAALUM - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, August 23, 2026

USHETU YATOA ZABUNI ZA SH. MILIONI 90.48 KWA MAKUNDI MAALUM


Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, mkoani Shinyanga, Bw. Mkali Kubebeka, amemweleza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Mwang’onda, kuwa Halmashauri hiyo imetoa zabuni zenye thamani ya shilingi milioni 90.48 (Sh. 90,478,100) kwa makundi maalum ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Bw. Kubebeka alitoa taarifa hiyo Agosti 22, 2026, katika Banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika viwanja vya Halmashauri hiyo.

Aliongeza kuwa Halmashauri imefanikiwa kusajili vikundi maalum 187, ambavyo viko tayari kuomba zabuni za umma kupitia Mfumo wa NeST.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa aliipongeza Halmashauri hiyo kwa hatua iliyofikia na kuitaka kuendelea kusajili vikundi zaidi na kuongeza zabuni zinazotengwa kwa ajili ya makundi maalum.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, inayozitaka taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi hayo.

“Nawapongeza pia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuhakikisha agizo hilo la Serikali ya Awamu ya Sita, ambalo pia ni takwa la Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, linatekelezwa ipasavyo,” alisema Mwang’onda.

Meneja wa PPRA Kanda ya Kati na Magharibi, Mhandisi Suma Atupele, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu na kuhamasisha umma ili Watanzania wengi zaidi wachangamkie fursa za zabuni za umma.

“Makundi ya vijana yanaweza kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi shilingi milioni 500. Kwa hiyo, hii si fursa ndogo. Kila Mtanzania ambaye hana uwezo wa kuanzisha kampuni ana nafasi ya kuunda kikundi na kuwa miongoni mwa wazabuni wanaopata zabuni na kujiinua kiuchumi,” alisema Mhandisi Atupele.

No comments:

Post a Comment