Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amewataka watumishi wa umma wanaoshiriki katika michezo kuzingatia maadili, nidhamu na heshima wanapokuwa katika viwanja vya michezo kama ilivyo katika Sheria za utumishi wa umma.
Mkomi ameyasema hayo leo Agosti 15,2026 Jijini Dodoma wakati akiongoza bonanza la uzinduzi wa Michezo ya shirikisho la michezo ya wizara na idara za serikali Tanzania ( shimiwi 2026) ambapo yanatarajiwa kuanza Septemba 20 mpaka Oktoba 7 mwaka huu mkoani Kilimanjaro.
"Serikali imeendelea kuhamasisha ushiriki wa watumishi katika michezo kupitia SHIMIWI, SHIMUTA na SHIMISEMITA kwa lengo la kuimarisha afya za wafanyakazi na kujenga mahusiano mazuri yatakayosaidia kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi,"amesema.
Aidha, amewaagiza waajiri katika taasisi za umma kuhakikisha wanatenga bajeti ya michezo na kuwawezesha watumishi kushiriki kikamilifu katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) yanayotarajiwa kufanyika mkoani Kilimanjaro kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 7 mwaka huu.
Amesema waajiri wanapaswa kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya michezo na kutoa kibali kwa watumishi wanaoshiriki mashindano hayo huku akimtaka Mwenyekiti na Katibu wa SHIMIWI kufuatilia taasisi ambazo hazitashiriki na kutoa taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe.
Kwa mujibu wa Katibu mkuu huyo amesema ushiriki wa watumishi katika michezo una umuhimu mkubwa katika kuimarisha afya, kujenga mshikamano na kuboresha mahusiano baina ya watumishi kutoka wizara, idara, mikoa na taasisi mbalimbali za Serikali.
“Licha ya kurudi na vikombe tunavyovitarajia, tuimarishe sana mahusiano mazuri baina yetu ili tuendelee kujenga utumishi wa umma kwa pamoja,” amesema, akisisitiza kuwa ushindani katika michezo usivunje udugu na mshikamano uliopo miongoni mwa watumishi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SHIMIWI Bw. Daniel Mwalusamba amesema bonanza hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango kazi na kalenda ya mwaka ya shirikisho huku akiwataka watumishi kuendelea kufanya mazoezi na kushiriki michezo kwa kuwa mazoezi ni muhimu katika kulinda na kuimarisha afya.
Naye Mkurugenzi wa huduma na biashara Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Bw.Rafael Makoninde amesema ushiriki wa watumishi katika michezo ni muhimu katika kujenga nguvu kazi yenye afya na tija huku akieleza kuwa OSHA itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha waajiri pamoja na wafanyakazi kuzingatia usalama na afya mahali pa kazi.
Amesema waajiri wanapaswa kutenga maeneo ya mazoezi kwa wafanyakazi wao ili kuwawezesha kufanya shughuli za kimwili, akibainisha kuwa mazoezi na michezo ni miongoni mwa njia zinazosaidia kukabiliana na changamoto za kiafya na kisaikolojia zinazoweza kuathiri utendaji wa wafanyakazi.
Bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguuna kuvuta kamba likiwa sehemu ya maandalizi ya mashindano ya SHIMIWI yatakayofanyika mkoani Kilimanjaro kuanzia Septemba 20 hadi Oktoba 7,2026 huku washiriki wakisisitizwa kuzingatia afya, mshikamano, ushindani wa haki na maadili ya utumishi wa umma.








No comments:
Post a Comment