Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Waziri Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa utekelezaji wa Mpango wa Matengenezo ya Barabara kwa Kutumia Vikundi vya Kijamii (CBRM) akieleza kuwa ni fursa muhimu ya kuwawezesha wananchi hususan vijana kushiriki katika shughuli za matengenezo ya barabara na kujiongezea kipato.
Mhe. Nanauka ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TARURA katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayoendelea katika uwanja wa Dkt. John Malecela mkoani Dodoma.
Amesema kuna umuhimu wa kuwafikia wananchi kwa kuwapa elimu ya kutosha kuhusu fursa zinazotolewa kupitia mpango wa CBRM ili waweze kushiriki kikamilifu. Aidha, amependekeza kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana na TARURA katika utekelezaji wa mpango huo.
"Ni muhimu kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika mpango wa CBRM. Pia napendekeza kuwepo kwa vikao vya mara kwa mara kati ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana na TARURA ili kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha malengo ya mpango huu yanafikiwa", amesema Mhe. Nanauka.
Kwa upande wake, Mratibu wa mpango wa CBRM TARURA Makao Makuu, Mhandisi Richard Missa amemueleza Waziri huyo kuwa Wakala umeanza utekelezaji katika mkoa wa Tanga, Morogoro,Dodoma na Pwani ambapo barabara zaidi ya kilomita 1500 zinahudumiwa na vikundi 302 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Aidha, amesema Wakala umejipanga kutekeleza mpango wa CBRM katika mikoa yote 25 ya Tanzania Bara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo zaidi ya kilomita 7000 za barabara zitafanyiwa matengenezo na vikundi 1100 vitapata fursa katika kazi hizo.
Mhandisi Missa amesema mpango huo unalenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika matengenezo ya kawaida ya barabara sambamba na kuchochea ajira na maendeleo ya kiuchumi katika jamii.
TARURA itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji na mafanikio ya mpango wa CBRM ili wananchi waendelee kunufaika na fursa zinazotokana na mpango huo.
Wakati huo huo, TARURA imewahimiza wananchi kuendelea kutembelea banda lake katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu kuhusu majukumu ya Wakala, ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu miundombinu ya barabara pamoja na kujionea mafanikio ya miradi inayotekelezwa nchini kwa lengo la kuimarisha maendeleo endelevu.



No comments:
Post a Comment