Na Okuly Julius, Dodoma.
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeeleza mafanikio mbalimbali iliyoyapata kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, kuanzia Agosti 1 hadi 8, 2026.
Akizungumza wakati wa kilele cha maonesho hayo, Afisa kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Asia Juma Abdallah, amesema ushiriki wa wizara hiyo umefanikiwa kuwafikia wananchi wengi na kutoa elimu kuhusu huduma na fursa zinazotokana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Bi. Asia amesema zaidi ya wananchi 3,000 walitembelea banda la wizara hiyo na kupata huduma pamoja na maelekezo kuhusu maeneo mbalimbali, ikiwemo usalama mtandaoni (cybersecurity), miundombinu ya TEHAMA, mifumo ya kidijitali na anwani za makazi.
“Zaidi ya wananchi 3,000 wametembelea banda letu na kupata huduma pamoja na maelekezo mbalimbali kuhusu shughuli zinazofanywa na idara zetu, zikiwemo za usalama mtandaoni, miundombinu, mifumo na anwani za makazi,” amesema Bi. Asia.
Bi. Asia amesema Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ina nafasi muhimu katika kuwezesha maendeleo ya taifa kupitia matumizi ya TEHAMA, huku ikilenga kuhakikisha Tanzania inaendelea kuelekea kwenye uchumi wa kidijitali sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
Ameeleza kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa ni Mkongo wa Taifa, ambao umewezesha kurahisisha mawasiliano na upatikanaji wa huduma za kidijitali ndani ya Serikali, taasisi zake na kwa wananchi kwa ujumla.
Aidha, amesema ujenzi wa minara zaidi ya 750 ya mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ambayo imezinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umeongeza upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ya vijijini.
Kwa mujibu wa Bi. Asia, huduma hizo zimekuwa na mchango katika kuwawezesha wananchi kutumia TEHAMA katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, afya na elimu, hivyo kuongeza ufanisi na tija.
Amesema wizara pia imekuwa ikitoa mafunzo kwa vijana na wanafunzi kuhusu matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones), roboti na Akili Bandia (AI) ili kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia hizo katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Ameongeza kuwa matumizi ya drones yanaweza kusaidia kurahisisha shughuli za kilimo na sekta nyingine, ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika uzalishaji.
Vilevile, amesema mifumo ya JamiiNamba na JamiiPay inaendelea kuchangia kurahisisha upatikanaji wa huduma na miamala mbalimbali, hatua inayosaidia kukuza uchumi wa kidijitali nchini.
Akizungumzia nafasi ya TEHAMA katika kukuza sekta ya kilimo, Bi. Asia amesema matumizi ya Akili Bandia (AI), sensa na mifumo ya kisasa ya umwagiliaji yanaweza kuongeza uzalishaji na tija, hivyo kuchangia ukuaji wa pato la taifa.
Amesema matumizi sahihi ya teknolojia yana nafasi kubwa katika kuwasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi, kuongeza ufanisi wa uzalishaji na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya kilimo.
Aidha, Bi. Asia amewataka vijana na Watanzania kwa ujumla kutumia fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia na mitandao ya kijamii kujenga uchumi wao badala ya kutumia muda mwingi katika shughuli zisizo na tija.
“Utajiri mkubwa hivi sasa uko kwenye mawasiliano. Watu waliounda majukwaa kama Facebook, Instagram na Twitter ni matajiri. Vijana wetu wasipoteze muda kwenye mambo yasiyo na tija; watumie vifaa vyao vya TEHAMA kujiongezea kipato kupitia biashara mtandaoni na fursa za kidijitali.”
Amesema Tanzania ina fursa kubwa katika uchumi wa kidijitali, hivyo vijana wanapaswa kutumia ubunifu, teknolojia na mitandao ya kijamii kuanzisha biashara, kutoa huduma na kutengeneza ajira kwao na kwa wengine.



No comments:
Post a Comment