BILIONI 1.8 KULIPA FIDIA KWA WAATHIRIWA 996 KUPISHA UJENZI WA BARABARA ZA LAMI WILAYANI RUANGWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 4, 2026

BILIONI 1.8 KULIPA FIDIA KWA WAATHIRIWA 996 KUPISHA UJENZI WA BARABARA ZA LAMI WILAYANI RUANGWA


Na Mwandishi Wetu - Ruangwa, Lindi


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi 996 ambao maeneo yao yameathiriwa na mradi wa ujenzi wa barabara mbili zenye urefu wa Km 59 kwa kiwango cha lami wilayani Ruangwa mkoani Lindi. 

Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Lindi, Mhandisi Alberto Kindole wakati wa zoezi maalumu la uhakiki wa taarifa za wananchi hao lililoanza tarehe 2 Septemba, 2026 wilayani Ruangwa kabla ya zoezi la malipo kuanza hivi karibuni.

Mhandisi Kindole amezitaja barabara hizo kuwa ni barabara ya Ruangwa-Nangugayi yenye urefu wa Km 31 na barabara ya Nandagala - Mpiluka- Nachingwea yenye urefu wa Km 31 ambazo zinatekelezwa kupitia mradi wa RISE unaogharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia. 

Amesema katika ujenzi wa barabara hizo kuna hatua mbalimbali zinazotakiwa kufanyika ili kuweza kujenga bila kupata vikwazo wakati wa utekelezaji wa mradi. 

"Kwa kulitambua hilo TARURA kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa pamoja na wadau wengine ilifanya tathmini kwa maana ya kupata idadi ya wale wanaoathiriwa na mradi", amesema Mhandisi Kindole.

Amesema barabara ya Ruangwa-Nangurugwayi ina wananchi watakaoathiriwa na mradi wapatao 581 wakati barabara ya Nandagala-Mpiluka-Nachingwea ina waathiriwa wa mradi 415 na kufanya idadi ya waathiriwa wa mradi huo kufikia 996 na wote wameshafanyiwa tathmini. 

Akizungumzia manufaa ya mradi huo, Mhandisi Kindole amesema mradi huo una faida nyingi na kubainisha kuwa maeneo yote yaliyopitiwa na mradi kuna uzalishaji mkubwa wa mazao kama vile korosho, ufuta, mbaazi na shughuli za uchimbaji wa madini ya aina mbalimbali.

Kwa upande wao, Bi. Rehema Mselemu na Bw. Hanafi Saidi ambao ni waathiriwa na wanufaika wa mradi huo wameridhishwa na mazoezi yote ya uthamini na uhakiki wa mali zilizopo katika maeneo yao yaliyoathiriwa na mradi lakini wamefurahishwa na uwepo wa mradi huo na kuiomba serikali itekeleze kwa haraka ili uweze kuwanufaisha hususan katika shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao yao kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

No comments:

Post a Comment