WATUMISHI NA WANANCHI WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUHARAKISHA MAENDELEO YA MOROGORO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 4, 2026

WATUMISHI NA WANANCHI WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUHARAKISHA MAENDELEO YA MOROGORO



Na Shua Ndereka, OKULY BLOG, Morogoro


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Cuthbert Sendiga, ametoa wito kwa watumishi wa umma, viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na wananchi wa Mkoa wa Morogoro kushirikiana kwa moyo mmoja katika kuleta maendeleo ya mkoa huo.

Sendiga ametoa wito huo Septemba 3, 2026, wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, ambapo alipokea rasmi kijiti cha uongozi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima.

Amesema mafanikio ya Mkoa wa Morogoro hayatatokana na juhudi za mtu mmoja, bali yatategemea ushirikiano, nidhamu, uwajibikaji na uzalendo wa kila mmoja.

Akizungumza katika hafla hiyo, Sendiga amesema Morogoro ni mkoa wenye fursa nyingi za maendeleo katika sekta za kilimo, mifugo, biashara, uwekezaji, utalii na maeneo mengine ya kimkakati, hivyo amewataka watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na ufanisi ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na maendeleo ya wananchi.

"Dhamira yangu ni kuhakikisha fursa hizi zinatumika ipasavyo ili maendeleo yawafikie wananchi, huduma za kijamii ziendelee kuboreshwa na mazingira ya kufanya kazi na kuwekeza yaimarishwe," amesema Sendiga.

Aidha, amesema katika hatua za uongozi wake atashughulikia suala la migogoro ya ardhi, kwani migogoro mingi ya ardhi husababishwa na baadhi ya wananchi kutofuata taratibu pamoja na uwepo wa baadhi ya viongozi wasiokuwa waaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Migogoro mingi ya ardhi nyuma yake inakuwa na baadhi ya viongozi wanaikingia kifua, mimi ninaomba tufanye kazi pamoja…kila raia wa nchi hii anapaswa kuheshimiwa na kupata haki yake na wezo wa kushughulikia migogoro ya ardhi tunao," amesema Sendiga.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi wa serikali za mitaa na kata kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi wa mazingira ili kuhakikisha Manispaa ya Morogoro na maeneo mengine ya mkoa yanakuwa safi na salama.

Queen Cuthbert Sendiga aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Agosti 27, 2026, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa akihudumu kama Mkuu wa Mkoa wa Manyara.




No comments:

Post a Comment