CDF, IGP MASHAHIDI KESI YA LISSU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 10, 2026

CDF, IGP MASHAHIDI KESI YA LISSU


Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es salaam, imeamuru Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuitwa mahakamani kutoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Uamuzi huo umetolewa leo, Septemba 10, 2026, na Jopo la Majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, huku Wajumbe wengine wa Jopo hilo ni Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Hata hivyo, Mahakama imekataa ombi la Lissu la kuwaita kutoa ushahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama na Ujasusi (DGIS).

Aidha, Mahakama imeridhia kuitwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camilius Wambura, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jacob Mkunda na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, kuwa mashahidi wa Lissu.

Lissu, ambaye pia ni Wakili, anakabiliwa na kesi ya uhaini akidaiwa kutenda kosa la kuitishia Serikali, kinyume na Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16, Toleo la 2022.

No comments:

Post a Comment