Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, imeeleza kuwa itaendelea kutengeneza barabara ya Singida–Manyara kwa hatua mbalimbali ili kuirudisha katika hali nzuri na kuwezesha huduma za usafiri na usafirishaji kufanyika kwa ufanisi.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, Septemba 29, 2026, alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Singida na Manyara.
Dkt. Msonde amesema Serikali tayari imeanza kutengeneza kilomita sita upande wa Singida na kilomita 15 upande wa Manyara, huku ikieleza kuwa matengenezo yataendelea katika sehemu nyingine za barabara hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha.
Amesema barabara hiyo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu kutokana na hali yake, hivyo Serikali imechukua hatua za makusudi kuhakikisha inafanyiwa matengenezo ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi na watumiaji wengine.
“Niwapongeze Mameneja wote wa Singida na Manyara kwa kuanza kuitengeneza barabara hii na kuirudisha katika hadhi yake. umuhimu wa barabara hii ni mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi wa mikoa ya Singida na Manyara,” amesema Dkt. Msonde.
Akiwa Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, Dkt. Msonde amewaeleza wananchi kuwa Serikali itaendelea na matengenezo ya barabara hiyo hadi kukamilika kwa sehemu zote zilizopangwa, huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika maeneo ambayo matengenezo yanaendelea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Almishi Hazali, ameiomba TANROADS Mkoa wa Manyara kuongeza kasi ya matengenezo ya barabara hiyo kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua, hususan katika maeneo ambayo tayari wameanza kuyafumua.
Aidha, amesema uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na viongozi wengine unaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutotupa taka kwenye mitaro na madaraja ili kuhakikisha maji yanapita kwa urahisi na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua.








No comments:
Post a Comment