TANZANIA, QATAR ZATIA SAINI MKATABA WA KUONDOA UTOZAJI KODI MARA MBILI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 29, 2026

TANZANIA, QATAR ZATIA SAINI MKATABA WA KUONDOA UTOZAJI KODI MARA MBILI.


Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kushoto) na Waziri wa Fedha wa Qatar, Mhe. Ali Bin Ahmed Al Kuwari, wakisaini Mkataba wa kuondoa utozaji kodi mara mbili (Double Taxation Agreement-DTA), kati ya mataifa hayo mawili, tukio lililofanyika kando ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia (AIIB) uliofanyika jijini Doha nchini Qatar.

Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kushoto) na Waziri wa Fedha wa Qatar, Mhe. Ali Bin Ahmed Al Kuwari, wakionesha hati za Mkataba wa kuondoa utozaji kodi mara mbili (Double Taxation Agreement-DTA), kati ya mataifa hayo mawili, mara baada ya kusaini hati hizo katika tukio lililofanyika kando ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia (AIIB) uliofanyika jijini Doha nchini Qatar.

Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kushoto) na Waziri wa Fedha wa Qatar, Mhe. Ali Bin Ahmed Al Kuwari, wakibadilishana hati za Mkataba wa kuondoa utozaji kodi mara mbili (Double Taxation Agreement-DTA), kati ya mataifa hayo mawili, mara baada ya kusaini hati hizo katika tukio lililofanyika kando ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia (AIIB) uliofanyika jijini Doha nchini Qatar.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Doha, Qatar)


TANZANIA na Qatar, leo tarehe 29 Septemba, 2026, zimetia saini Mkataba wa Kuepusha utozaji kodi mara mbili na kuzuia ukwepaji kodi (Double Taxation Agreement).

Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) na Waziri wa Fedha wa Qatar, Mhe: Ali Bin Ahmed Al Kuwari, wamesaini Mkataba huo kando ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia (AIIB) uliofanyika jijini Doha nchini Qatar.

Mhe. Balozi Omar amesema kuwa hatua hiyo imelenga kuboresha mazingira ya biashara kati ya mataifa hayo mawili, hatua itakayo kuza zaidi uchumi wa pande zote mbili.

"Mkataba huu unaakisi urafiki imara uliopo kati ya mataifa yetu mawili, pamoja na azma yetu ya kujenga mfumo wa kisasa, wenye usawa na unaovutia wawekezaji, unaoendana na viwango vya kimataifa." Alisema Mhe. Balozi Omar.

"Kwa kuondoa utozaji kodi mara mbili, mkataba huu utachagiza biashara ya kimataifa, uwekezaji na shughuli za kibiashara. Pia utajenga mazingira ya uwazi na yanayotabirika zaidi kwa wawekezaji," alisema Mhe. Balozi Omar.

Aliongeza kuwa, mkataba huo unaimarisha ushirikiano kati ya mamlaka za kodi za nchi zote mbili na utasaidia juhudi za kimataifa za kupambana na ukwepaji na upunguzaji wa kodi, pamoja na kulinda maslahi ya kodi ya nchi zote mbili.

Alitaja sekta ambazo Tanzania inatarajia kuvutia uwekezaji mpya kuwa ni pamoha na miundombinu, nishati, utalii, usafirishaji na vifaa, kilimo na huduma za fedha.

"Tanzania inautazama mkataba huu kama fursa ya kuvutia uwekezaji mpya katika sekta mbalimbali" alisema Mhe. Balozi Omar

Aidha, alizishukuru timu za kiufundi, wataalam wa kodi, washauri wa kisheria na maafisa wa serikali kutoka nchi zote mbili, akisema kujitolea kwao ndiyo kumewezesha mafanikio hayo.

Aliongeza kuwa nchi zote mbili sasa zinatazama utekelezaji wa haraka wa mkataba huo na ushirikiano wa kiuchumi uliozidi kuwa wa kina kwa manufaa ya pamoja ya wananchi wa nchi zote mbili.

Kwa upande wa biashara, alisema kuondolewa kwa utozaji kodi mara mbili katika mapato, kunatarajiwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa kampuni zinazofanya kazi katika nchi zote mbili, na kuweka mazingira ya uhakika zaidi kwa wawekezaji wanaotaka kupanua shughuli zao katika mataifa hayo.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha wa Qatar, Mhe: Ali Bin Ahmed Al Kuwari, alisema kuwa Tanzania ni mshirika muhimu wa kiuchumi wa Qatar na kwamba kuondolewa kwa vikwazo vya utozaji kodi mara mbili katika mapato yanayotokana na biashara zinazofanyika kati ya mataifa hayo mawili kutavutia zaidi uwekezaji na mitaji kutoka katika nchi hizo.

Amesisitiza nia ya nchi yake kuendeleza ushirikiano wa karibu na Tanzania, akibainisha kuwa Mamlaka ya Uwekezaji ya Qatar (QIA) na Mfuko wa Maendeleo wa Qatar (QFFD) tayari wanashiriki katika miradi mbalimbali nchini humo.

Alieleza utayari wa Qatar kusaidia katika ubadilishanaji wa maarifa na utaalamu, badala ya kuhamisha maarifa pekee.

Mhe: Ali Bin Ahmed Al Kuwari aligusia umuhimu wa ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi na kwamba kuwepo kwa mikataba ya kuzuia utozaji kodi mara mbili ni muhimu kwa miradi iliyotekelezwa tayari nchini Tanzania na miradi mipya kutoka nchi hizo mbili.


No comments:

Post a Comment