Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
KAMATI ya Kudumu ya Masuala Mtambuka ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) imeipongeza Tanzania kwa maendeleo ya vituo vya umahiri katika huduma za tiba, elimu na mafunzo ya magonjwa ya moyo, ikisema uwepo wa vituo hivyo unaweza kupunguza utegemezi wa wananchi wa Afrika Mashariki kwenda nje ya bara kutafuta matibabu.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mary Mugyenyi, baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutembelea vituo vya umahiri vya Afrika Mashariki katika maeneo ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, meno na kinywa pamoja na mfumo wa damu.
Vituo hivyo vinatarajiwa kuwa chini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH).
Mugyenyi amesema ziara hiyo imeiwezesha kamati kushuhudia maendeleo makubwa katika elimu, mafunzo na huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo nchini, huku teknolojia mbalimbali zikitumika katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Amesema uwepo wa vituo hivyo ndani ya Afrika Mashariki utasaidia wananchi kupata huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo ndani ya ukanda huo, badala ya kusafiri kwenda nchi kama India, Uturuki na mataifa mengine kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa Mugyenyi, hatua hiyo pia itasaidia kuimarisha uwezo wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, pamoja na kuongeza fursa za mafunzo kwa wataalamu wa afya.
Amesema EALA itaendelea kuhamasisha wananchi wa Afrika Mashariki kufahamu na kutumia huduma zinazotolewa kupitia vituo hivyo, ikiwemo huduma za matibabu, elimu na mafunzo katika eneo la magonjwa ya moyo.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa EALA walishuhudia maendeleo ya uwekezaji katika vituo hivyo na kupata maelezo kutoka kwa viongozi wa taasisi husika kuhusu namna huduma hizo zitakavyowanufaisha wananchi wa Tanzania na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Naizihijwa Majani, amesema maendeleo ya kituo hicho yanaendelea kuongeza uwezo wa Tanzania katika kutoa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. Emmanuel Balandya, ameeleza umuhimu wa vituo hivyo katika kuunganisha huduma za matibabu na mafunzo ya wataalamu ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Wajumbe wa EALA, akiwemo Ansar Kachwamba kutoka Tanzania na Jacqueline Amongin kutoka Uganda, wameeleza kuwa uwekezaji huo ni muhimu katika kuimarisha huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wananchi wa nchi wanachama.
Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya afya na kuongeza uwezo wa Afrika Mashariki kujitegemea katika huduma za matibabu na mafunzo ya kitaalamu.
















No comments:
Post a Comment