VIONGOZI mbalimbali walioshiriki Mkutano wa Kimataifa ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kuhusu utekelezaji wa Afya Moja katika mifumo ya chakula na kilimo wameazimia kuwe na uzalishaji mkubwa wa chanjo za sotoka ili kudhibiti ugonjwa huo kwa haraka.
Aidha, walisisitiza haja ya kuwa na uwekezaji mkubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo, matumizi ya mbinu za kisayansi, tafiti za kisayansi na uwepo wa maabara za kisasa zenye wataalamu wa kutosha.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba alisema kuna haja ya kuwa na uwekezaji wenye nguvu zaidi, unaotabirika na endelevu na kuahidi kwamba Tanzania imejizatiti kushiriki katika juhudi za kimataifa za kutokomeza sotoka ifikapo mwaka 2040.
“Umiliki wa kitaifa na ufadhili wa ndani lazima viwe msingi, vikisaidiwa na FAO, WOAH, Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda, taasisi za fedha za kimataifa, washirika wa maendeleo na sekta binafsi,” alisema.
“Tunapaswa kuondoka katika hatua zilizotawanyika na kuelekea kwenye mifumo ya kudumu; kutoka mipango ya kitaifa pekee kwenda ushirikiano wa kikanda; na kutoka ahadi kwenda kwenye matokeo yanayoweza kupimika,” alisisitiza.
Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Bw. Godfrey Magwenzi alisema tayari nchi mbalimbali zimemepata somo muhimu kutokana na kutokomezwa kwa rinderpest (sotoka ya ng’ombe) ambayo ilihitimishwa mwaka 2011.
“Kwa upande wa sotoka, tunayo maarifa, zana na ushirikiano wa kimataifa unaohitajika ili kutokomeza ugonjwa huu. Changamoto iliyopo ni kuhakikisha uwekezaji wa muda mrefu unaofikisha huduma na hatua zinazohitajika hadi maeneo ya mwisho.”
“Uwekezaji wa kimkakati unaweza kuleta matokeo ya kudumu. Hii ni kwa sababu zana, sayansi, ushirikiano na dhamira ya kisiasa tayari vipo. Kinachohitajika sasa ni uwekezaji wa kutosha ili kubadili dhamira hiyo ili tupate matokeo halisi,” alisema.
Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Ulaya jijini Roma na Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja huo katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya Roma, Dkt. Martin Selmayr, alisema jumuiya zote zinapaswa kujifunza kutokana na mafanikio yaliyopatikana wakati kutokomeza rinderpest.
“Ushirikiano wa kimataifa, sayansi na chanjo ulifanya iwezekane. Kwa sotoka ya kondoo na mbuzi, tunahitaji mtazamo mpya. Hatupaswi kuishia katika kampeni nyingine ya chanjo pekee. Tunapaswa kutumia Global Gateway kama kichocheo cha uwekezaji.”
Balozi Selmayr alisema nchi washirika zinapaswa kuwekeza rasilimali zao katika programu za kitaifa za kutokomeza ugonjwa; benki za maendeleo na taasisi za fedha za kimataifa zinapaswa kushiriki; madaktari binafsi wa mifugo, wazalishaji wa chanjo na sekta binafsi wanapaswa kushiriki katika uwekezaji na utoaji wa huduma pia nchi zinahitaji kuimarisha ushirikiano wa kuvuka mipaka.
Naye, Mkurugenzi wa Timu ya Mifugo wa taasisi ya The Gates Foundation, Dkt. Samuel Thevasagayam alisema uzoefu uliopatikana kwenye kampeni ya kutokomeza rinderpest utumike kusaidia kuhamasiaha rasilmali zaidi ili kutokomeza sotoka ya mbuzi na kondoo.
“Uzoefu wa rinderpest unatufundisha kwamba tunapofikia hatua ya mwisho, tunapaswa kuhamasisha rasilimali ili kumaliza kazi, badala ya kurudia kampeni bila mkakati wa kufikia mwisho. Tunahitaji nidhamu na utekelezaji unaolenga kufikia mwisho,” alisema.
Dkt. Thevasagayam alisema taasisi ya Gates Foundation iko tayari kushirikiana na Umoja wa Ulaya na nchi mbalimbali, na kutumia rasilimali zake kama kichocheo ili nchi ziongeze ahadi na uwekezaji wao wenyewe.
Akielezea kuhusu mafanikio ya Tanzania kushiriki kwenye mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo alisema mijadala katika mkutano huo ilijikita katika kubadili mtazamo wa afya kutoka kuwa sekta inayojitegemea na badala yake kuiona kama sehemu ya mnyororo mzima wa uzalishaji wa chakula na mifugo.
Alisema kuwa mijadala hiyo ilijikita kuona namna ya kuimarisha mnyororo wa uzalishaji, ikiwemo udhibiti wa magonjwa ya mifugo barani Afrika, yakiwemo Sotoka pamoja na Ugonjwa wa Midomo na Miguu.(Foot and Mouth Disease – FMD).
Alisema kuwa, hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha afya inalindwa kuanzia kwenye uzalishaji wa kilimo na ufugaji hadi kwenye bidhaa zinazomfikia mlaji. “Unaweza ukaona mkutano umekuwa na tija kubwa, kwa sababu sasa tunazungumza afya katika mnyororo na siyo katika vipande vipande.”
Aliongeza kuwa dhana hiyo ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania kwa kuwa usalama wa afya ya mifugo una mchango wa moja kwa moja katika upatikanaji wa virutubisho muhimu kwa binadamu, huku usalama wa chakula ukitegemea pia mifumo salama ya uzalishaji.






No comments:
Post a Comment