Na Ssgt Mawazo Mtondo - MWANZA.
Mkuu wa Ofisi ya Michezo na Utamaduni Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Solomon Mwambingu, leo 19 Septemba, 2026, ameeleza maandalizi na mikakati ya Jeshi la Magereza kuelekea Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) 2026.
ACP Mwambingu ameyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), jijini Mwanza, ambapo amesema Jeshi la Magereza limejiandaa vyema katika michezo mbalimbali kuelekea mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 21 hadi Oktoba 5, 2026, katika Viwanja mbalimbali, jijini Mwanza.
Amesema kama sehemu ya maandalizi, Jeshi la Magereza lilifanya Mashindano ya CGP CUP jijini Dar es Salaam mwezi Agosti 2026, kwa lengo la kuziandaa timu na kuhakikisha zinafikia kiwango kizuri cha ushindani kuelekea BAMMATA.
“Jeshi la Magereza limejiandaa vyema katika michezo mbalimbali. Tunaendelea kuibua na kukuza vipaji, ambapo Kocha wa Timu ya Taifa ya Netiboli anatoka Jeshi la Magereza, pamoja na kuwa na wachezaji wanaowakilisha timu za taifa. Tumejiandaa vyema na tupo tayari kushindania vikombe katika BAMMATA 2026,” amesema ACP Mwambingu.
Aidha, ACP Mwambingu aliendelea kueleza kuwa ufunguzi na ufungaji wa Mashindano hayo utafanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, pia alitaja Viwanja vingine vitakavyotumika kwa ajili ya mashindano hayo pamoja na michezo husika itakayofanyika, alisema Uwanja wa CCM Kirumba utatumika wa michezo ya Mpira wa Pete (Netball), Riadha na Mpira wa Miguu (Football), pamoja na kufanyika kwa shughuli za ufunguzi na ufungaji wa mashindano. Uwanja wa Chuo cha Ualimu Butimba kutafanyika michezo ya Mpira wa Miguu (Football), Mpira wa Pete (Netball) na Mpira wa Kikapu (Basketball). Viwanja vya Milongo kutafanyika michezo ya Mpira wa Mikono (Handball), Mpira wa Kikapu (Basketball) na Mpira wa Wavu (Volleyball). Viwanja vya MTC kutafanyika mchezo wa Shabaha.
Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) ni chombo cha kitaalamu cha michezo kilichosajiliwa kwa lengo la kusimamia na kuratibu shughuli za michezo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
BAMMATA lilianzishwa rasmi mwaka 1977 na linajumuisha Kanda nane ambazo ni Kanda ya Ngome, Kanda ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kanda ya Polisi, Kanda ya Magereza, Kanda ya Uhamiaji, Kanda ya Zimamoto na Uokoaji, Kanda ya Visiwani na Kanda ya SMZ.





No comments:
Post a Comment