Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema matumizi ya teknolojia ya kidijitali yamekuwa muhimu katika nyanja mbalimbali, ikiwamo biashara, elimu na huduma za kijamii na Serikali, huku wananchi wakitumia mifumo ya kidijitali kufanya malipo na kupata huduma.
Waziri Kairuki amyeasema hayo leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza ziara aliyoifanya Kituo Jumuishi cha TTCL cha huduma za faiba kilichopo Kijitonyama ambapo amesema mageuzi makubwa ya kidijitali yanaongeza umuhimu wa huduma za TTCL kwa wananchi.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa miaka 10 wa mageuzi ya kidijitali kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaelewa na kutumia teknolojia hizo, sambamba na kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kidijitali.
Waziri Kairuki amesema Tanzania imefikia kiwango cha asilimia 47 cha matumizi ya simu janja na kwamba Serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya mawasiliano kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata vifaa vinavyowawezesha kutumia huduma za kidijitali.
“Vitakuwa havina maana kwamba TTCL pamoja na mitandao mingine ya mawasiliano ya simu inaweka huduma hizi, halafu wateja wenyewe hawawezi kuzitumia, tuendelee kuhakikisha tunatangaza huduma zinazopatikana ili wananchi wazielewe na kuzitumia” amesema.
Hata hivyo Waziri Kairuki amesema TTCL limepiga hatua katika utekelezaji wa huduma ya intaneti ya kasi kupitia teknolojia ya Faiba Mlangoni Kwako (FTTH), huku ikipanua huduma hiyo katika nyumba za kisasa kupitia mfumo wa Smart Home.
Amesema utekelezaji wa awamu ya kwanza ya FTTH umeonesha mafanikio makubwa baada ya kuwafikia na kuwaunganisha wateja wengi, hatua iliyoliwezesha shirika hilo kuanza awamu ya pili ya huduma hiyo.
Aidha amesema pamoja na huduma ya fiber majumbani, TTCL imeendelea kupanua matumizi ya teknolojia hiyo katika maeneo mbalimbali, ikiwamo ofisi kupitia huduma zinazolenga kupeleka muunganisho wa faiba karibu zaidi na mtumiaji.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, TTCL imeanza pia kuunganisha huduma za fiber na teknolojia za Smart Home, zinazolenga kuwezesha nyumba kutumia mifumo mbalimbali ya kidijitali kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi.
“Tunawakaribisha sana Watanzania wote, kwa rika zote. TTCL imejipanga vizuri sana na tumeshafanya mambo makubwa. Sasa hivi siyo TTCL ambayo mmeijua ya wakati ule, imebadilika sana katika utoaji wa huduma zake,” amesema.
Waziri Kairuki amesema changamoto katika utoaji wa huduma haziwezi kukosekana, hasa kutokana na ongezeko la idadi ya watumiaji, lakini amesisitiza kuwa TTCL imeendelea kuboresha mifumo yake, ikiwamo eneo la huduma kwa wateja huku akisisitiza uwepo wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeendelea kuwa sehemu muhimu katika kuongeza kasi ya utoaji wa huduma za intaneti, huku gharama za huduma zikipungua.
Aidha, amesema TTCL imezindua huduma ya Triple Hub, inayowawezesha watumiaji kupata huduma kupitia vifaa mbalimbali, ikiwamo simu za mkononi, kompyuta mpakato pamoja na simu za mezani.
Amesema huduma hiyo inaweza kutumiwa na wanafamilia waliopo maeneo tofauti kwa kutumia kifurushi kimoja, akitoa mfano wa mwanafamilia aliyepo Dar es Salaam, mwingine Dodoma na mwingine Mbeya.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa amesema shirika hilo limeweka mpango wa kuongeza maungio ya huduma ya intaneti ya faiba mlangoni kwako hadi kufikia takribani 750,000 ifikapo Juni 2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Amesema kwa sasa shirika hilo limejenga maungio takribani 330,000 yanayowezesha nyumba na maeneo mbalimbali kufikiwa na huduma hiyo, huku wateja wapatao 115,000 wakiwa tayari wamejiunga na mtandao huo.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, TTCL inalenga kujenga maungio mengine takribani 400,000, hatua ambayo itafanya idadi ya maungio kufikia karibu 750,000 katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Marwa, TTCL kwa sasa inatumia teknolojia ya GPON katika utoaji wa huduma hiyo, ambayo imewezesha shirika kuwafikia wateja wengi zaidi kwa wakati mmoja ikilinganishwa na teknolojia ya awali ya point-to-point.
Amesema TTCL inaendelea kuwekeza katika huduma ya faiba mlangoni kwa lengo la kubaki kinara katika eneo hilo, huku ikitumia pia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaosimamiwa na shirika hilo kufikisha huduma kwa wananchi majumbani na maofisini.
Marwa amesema uwekezaji huo unalenga kuhakikisha miundombinu iliyowekwa na Serikali inawanufaisha wananchi moja kwa moja, hususan katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kuimarisha uchumi wa kidijitali.
Ameongeza kuwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali yamepewa uzito katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo TTCL itaendelea kujenga miundombinu na kuunganisha wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi huo.






No comments:
Post a Comment