
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tanga, Jabir Singano, amewataka wakazi wa Wilaya ya Muheza kujitokeza kwa wingi katika Kliniki ya Ardhi inayoendelea wilayani humo, ili kupata huduma, elimu na ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi.
Singano amesema lengo la Kliniki hiyo ni kusogeza huduma za ardhi karibu zaidi na wananchi na kuziunganisha kwa pamoja, ili wananchi waweze kupata huduma wanazohitaji kwa urahisi, pamoja na kupata elimu kuhusu taratibu mbalimbali za masuala ya ardhi.

Ameongeza kuwa Kliniki hiyo inatoa fursa kwa wananchi wenye changamoto au migogoro ya ardhi kupata ushauri na kuelekezwa taratibu sahihi za kufuata, huku wataalamu wakiwa tayari kuwasikiliza na kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zao.

Kwa upande wake, Haruna Ali, mkazi wa Muheza, ameshukuru kwa kupata hati yake baada ya kusubiri kwa muda mrefu, akisema tangu mwaka 2020 alikuwa akisikia taarifa za watu kutajwa kuchukua hati, lakini yeye hakuwahi kupigiwa simu wala kupewa taarifa.

Amesema huduma hiyo imempa faraja na ameomba iendelee ili kuwasaidia wananchi wengine ambao bado hawajapata hati zao. Aidha, amewataka wananchi wenye changamoto za hati kutumia fursa hiyo kupata maelekezo na msaada kutoka kwa wataalamu ili waweze kukamilisha taratibu zinazohitajika.

Naye Hatibu Mwijuma, mkazi wa Muheza, amewashukuru viongozi wa Mkoa wa Tanga na Wilaya ya Muheza, pamoja na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tanga na timu yake, kwa kusogeza huduma hizo karibu na wananchi na kuwezesha upatikanaji wa hati.

Mwijuma amesema alikamilisha taratibu za kupata hati wiki iliyopita na baada ya kupata taarifa kuhusu Kliniki ya Ardhi iliyofanyika Muheza, alifika na kufanikiwa kukabidhiwa hati yake baada ya kukamilisha vigezo vilivyohitajika.

Ameiomba Wizara ya Ardhi kuendelea na utaratibu wa kupeleka huduma karibu na wananchi, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza kero na migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kliniki ya Ardhi katika Wilaya ya Muheza inafanyika kwa siku tano, kuanzia tarehe 22 hadi 26 Septemba 2026, ikiwa na lengo la kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kutoa elimu pamoja na ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi.


No comments:
Post a Comment