MADAKTARI BINGWA WA BMH WAWASILI NCHINI MALAWI KWA AJILI YA KAMBI YA MATIBABU YA KIBOBEZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, September 28, 2026

MADAKTARI BINGWA WA BMH WAWASILI NCHINI MALAWI KWA AJILI YA KAMBI YA MATIBABU YA KIBOBEZI



Na Mwandishi Wetu LILONGWE, MALAWI


Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wamewasili nchini Malawi kwa ajili ya kambi maalumu ya matibabu.

 Madaktari hao ambao wamewasili, wamepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes Richard Kayola, aliyeikaribisha Timu hiyo na kuitakia mafanikio katika utoaji wa huduma.

Akizungumza wakati wa mapokezi, Balozi Kayola amesema kambi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi na Utalii Tiba inayotokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba vya Kisasa na wataalamu bingwa. 

Ameongeza kuwa kambi hiyo pia itatoa fursa ya kubadilishana uzoefu wa kimatibabu baina ya madaktari wa Tanzania na Malawi. 

Aidha, alifahamisha kuwa mwisho wa Kambi hii inategemewa utasainiwa Mkataba utakaowezesha wagonjwa wenye kuhitaji huduma zaidi kusafirishwa na kwenda nchini Tanzania kupata huduma kulingana na mahitaji husika.

Kwa upande wake, kiongozi wa msafara huo, Bi. Monica Kessy, amesema madaktari wote wamewasili salama na wako tayari kutoa huduma kwa wananchi wa Malawi, huku akibainisha kuwa utoaji wa huduma utaongozwa na hospitali husika watakazofanyia kazi.

Kambi hiyo imeanza tarehe 28/09/2026 na inategemewa kumalizika tarehe 9/10/2026, ikitoa huduma za kibingwa katika upasuaji wa mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu, matibabu ya magonjwa ya moyo na mfumo wa mkojo, pamoja na tathmini kwa ajili ya upandikizaji wa figo.







No comments:

Post a Comment