MAISHA MAPYA NJE YA GEREZA, CHEREHANI YAMFUNGULIA ISSA NJIA YA KUJITEGEMEA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 8, 2026

MAISHA MAPYA NJE YA GEREZA, CHEREHANI YAMFUNGULIA ISSA NJIA YA KUJITEGEMEA




Na Shua Ndereka, OKULY BLOG, Morogoro


Taasisi ya The Islamic Foundation yenye Makao yake Makuu Mkoa wa Morogoro, imetoa msaada wa cherehani kwa Issa Mohamed Kitambi, aliyemaliza kifungo cha miaka minane katika Gereza la Mahabusu Morogoro, ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono katika kuanza maisha mapya baada ya kutoka gerezani.

Issa ambaye alipata mafunzo ya ushonaji akiwa gerezani, sasa anatarajiwa kutumia cherehani hiyo kuendeleza ujuzi alioupata na kujiajiri kupitia kazi ya ushonaji wa nguo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa The Islamic Foundation, Arafat Badru, amesema wameguswa na jitihada zinazofanywa na Jeshi la Magereza za kuwapatia wafungwa mafunzo ya ujuzi, ili wanapomaliza vifungo vyao wawe na uwezo wa kujitegemea.

Amesema cherehani hiyo imelenga kumpa Issa nyenzo ya kuanzia katika kazi yake na kumsaidia kuendesha maisha yake baada ya kumaliza kifungo.

Akizungumza katika zoezi hilo, Mkuu wa Gereza la Mahabusu Morogoro, Mrakibu wa Jeshi la Magereza SabaSaba Mselemu, amesema Issa alitumia miaka mitatu akiwa gerezani kupata mafunzo ya ushonaji yaliyotolewa kwa ushirikiano na Chuo cha VETA Kihonda Morogoro.

Amesema mafunzo hayo yamekuwa na umuhimu mkubwa katika kuwaandaa wafungwa kwa maisha ya nje ya gereza, kwa kuwapatia ujuzi unaoweza kuwasaidia kujiajiri.

“Mwanafunzi wetu Mussa Kitambi, amemaliza kifungo chake cha miaka nane gerezani, kwa kushirikiana na VETA, Gereza la mahabusu Morogoro, na Taasisi ya Islamic foundation tumeweza kumpatia cheti na cherehani cha kuanzia Maisha huko anakokwenda”. Alisema Mselemu

Aidha Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kihonda Fred Uriki, amesema chuo hicho kimeanzisha ushirikiano na Jeshi la Magereza kwa lengo la kuwafundisha wafungwa katika fani mbalimbali za ufundi ambapo lengo la mafunzo hayo, ni kuwawezesha wafungwa wanapomaliza vifungo vyao kutumia ujuzi walioupata kujiajiri, kuanzisha shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato.

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza Peter Anatory, amesema kazi ya Jeshi la Magereza si kuwahifadhi wafungwa pekee, bali ni kuwasaidia kurekebika na kuwaandaa kurejea katika jamii wakiwa raia wema.

Pia amesema, kuwapatia mafunzo ya ujuzi ni moja ya njia zinazosaidia kuwajengea uwezo wa kuishi maisha ya kawaida na kufanya shughuli halali baada ya kumaliza vifungo vyao.

Naye Issa Mohamed Kitambi amelishukuru Jeshi la Magereza kwa kumpatia fursa ya kujifunza ushonaji pamoja na The Islamic Foundation kwa kumpatia cherehani hiyo kwani, msaada huo utamsaidia ni chanzo cha kipato katika maisha yake mapya, huku akiahidi kutumia fursa hiyo kwa manufaa yake na jamii kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment