MALEZI BORA MSINGI WA KUJENGA KIZAZI CHENYE MAADILI NA UWAJIBIKAJI – NAIBU WAZIRI MAHUNDI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, September 20, 2026

MALEZI BORA MSINGI WA KUJENGA KIZAZI CHENYE MAADILI NA UWAJIBIKAJI – NAIBU WAZIRI MAHUNDI


Na WMJJWM – Arusha


Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Winfred Mahundi, amewataka wazazi, walezi, walimu na jamii kuimarisha ushirikiano katika malezi na makuzi ya watoto, akisisitiza kuwa malezi bora ni msingi wa kujenga kizazi chenye maadili, nidhamu, uwajibikaji na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali katika jamii ya sasa.

Ameyasema hayo Septemba 19, 2026, jijini Arusha wakati wa Mahafali ya 12 ya Darasa la Saba na Mahafali ya 8 ya Kidato cha Nne katika Shule ya St. Monica Moshono.

Mhe. Mahundi amesema malezi ya mtoto hayapaswi kuangalia mafanikio ya kitaaluma pekee, bali yanapaswa kuzingatia makuzi na ukuaji wa kimwili, kiroho, kitabia na kitaaluma, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya mtoto yanahitaji ushirikiano wa familia, shule, jamii na Serikali.

Amesema wazazi na walezi wana wajibu wa kuwa karibu na watoto wao, kuwafuatilia, kuwasikiliza na kuwapatia mwongozo unaofaa ili kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika maisha.

“Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kushirikiana na jamii katika kujenga mazingira yenye ulinzi, haki, usalama na fursa kwa watoto, Aidha, mabadiliko ya teknolojia yameleta fursa mbalimbali kwa watoto katika kujifunza na kupata taarifa, lakini pia yameibua changamoto zinazohitaji uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi, walezi na walimu hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuwaongoza watoto katika matumizi sahihi ya teknolojia na kuwajengea uwezo wa kutambua taarifa na maudhui yenye manufaa na yale yanayoweza kuwa na madhara katika maisha yao, pamoja na kuhakikisha matumizi ya teknolojia hayaathiri maadili, nidhamu na mwenendo wa watoto.” Alisesema Naibu Waziri Mahundi

Awali, akisoma taarifa ya shule hiyo, Mkuu wa shule hiyo Sr. Yuster Andrea Mbilinyi amesema shule imeendelea kuweka mkazo katika elimu, malezi na makuzi ya wanafunzi ili kuwajenga kuwa watu wenye nidhamu, maadili na uwajibikaji katika jamii.

Sr. Yuster ameongeza kwamba pamoja na kufanya vizuri kitaaluma, shule imeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na malezi kwa wanafunzi kwa kuweka miundombinu ya kujifunzia na mazingira ya shule 

Amesema ushirikiano wa wazazi na shule ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata malezi na matunzo yanayowawezesha kukua katika mazingira salama, huku akiwataka wazazi kuendelea kufuatilia maendeleo ya watoto wao na kushirikiana na walimu katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Serikali itaendelea kushirikiana na jamii katika kuimarisha mazingira yanayolinda na kukuza ustawi wa watoto, ili kuhakikisha wanapata malezi, elimu na fursa zinazowawezesha kukua na kuwa raia wenye mchango katika maendeleo ya familia, jamii na Taifa.

No comments:

Post a Comment