![]() |
| Afisa Mtendaji Mkuu wa Hazina Saccos, Dkt. Festo Sanga akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Hazina Saccos uliofanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Morena Hotel Mjini Morogoro. |
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) ameiagiza Menejiment ya Hazina Saccos kuhakikisha fedha za wanachama zinalindwa kwa kiwango cha juu, huku akiwataka kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, ukaguzi wa ndani na udhibiti wa mikopo pamoja na urejeshaji wake.
Mhe. Munde aliyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 13 wa Hazina Saccos Ltd uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Morena, Mjini Morogoro.
Mhe. Munde alisema kuwa ili chama kiwe imara ni muhimu kiwe na mfumo mzuri wa ukaguzi wa ndani ambao utajumuisha usimimizi wa vihatarishi na kuendelea kuimarisha usalama wa mifumo na usiri wa taarifa za wanachama, sambamba na kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya huduma hizo.
‘’Ninawaelekeza viongozi na Menejimenti ya Hazina SACCOS kuhakikisha kuwa, fedha za Wanachama zinalindwa kwa kiwango cha juu. Kila muamala lazima uwe na nyaraka stahiki, uthibitisho na ufuatiliaji unaostahili’’. Alisema Mhe. Munde
Mhe. Munde aliongeza kuwa ili kufikia mafanikio Hazina Saccos inatakiwa kuongeza juhudi za kuwafikia vijana, wanawake na makundi mengine ambayo bado hayajatumia kikamilifu huduma za kifedha ili makundi hayo yaweze kujikwamua kiuchumi.
Aidha, Mhe. Munde alisema kuwa serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na vyama vya ushirika na Saccos katika kukuza uchumi wa wananchi.
‘’Serikali inatambua kuwa Vyama vya Ushirika na SACCOS vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi. Kupitia SACCOS wananchi wanaweza kuweka akiba, kupata mikopo kwa masharti nafuu, kukuza biashara na kuimarisha ustawi wa familia’’. Aliongeza Mhe. Munde.
Pia, Mhe. Munde alitumia mkutano huo kuwataka Wanachama wa Hazina Saccos kutimiza wajibu wao kwa kuweka akiba kwa utaratibu na kurejesha mikopo kwa wakati na kuwasisitiza kuwa SACCOS haiwezi kukua ikiwa Wanachama hawataweka akiba na kutimiza masharti ya mikopo.
Awali akiongea kwenye Mkutano huo Afisa Mtendaji Mkuu wa Hazina Saccos, Dkt. Festo Mwaipaja alisema mkutano mkuu wa 13 unatoa fursa ya kutathmini chama kilipotoka, kilipo na kinapotaka kwenda, hivyo mkutano huo utatumika kujadili taarifa mbalimbali za chama.
Dkt. Mwaipaja aliwataka wanachama kushiriki kikamilifu na kutoa maoni kwa uwazi, nidhamu na heshima na kuwahakikishia wanachama kuwa kila hoja itazingatiwa kwa maslahi mapana ya Hazina Saccos na wanachama wake.
‘’Mkutano huu wa 13 unatupa fursa ya kutathmini tulikotoka, tulipo na tunakotaka kwenda. Tutapokea na kujadili taarifa mbalimbali, kupitia hali ya kifedha ya Chama, kutathmini utekelezaji wa maamuzi ya mikutano iliyopita na kuweka vipaumbele vya kipindi kijacho’’. Alisema Dkt. Mwaipaja.
Dkt. Mwaipaja aliongeza kuwa Chama kimeendelea kuimarisha utamaduni wa kuweka akiba, kutoa huduma za mikopo, kusimamia marejesho, kulinda mali zake na kuboresha mifumo ya ndani hatua ambazo zimeendelea kuifanya Hazina Saccos kuwa miongoni mwa Taasisi ya Kifedha imara, inayotegemewa na inayoweka maslahi ya wanachama mbele.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Bodi wa Hazina Saccos, Bi.Neema Mwakitalima alisema kuwa Hazina Saccos imeendelea kukua kwa kasi na kutoa huduma za kifedha kwa wanachama zaidi ya elfu kumi na moja kutoka mafungu (Vote) 432 serikalini.
Bi. Mwakitalima aliongeza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Agosti 2026, jumla ya Wanachama 1,367 walijiunga na Chama, na kufanya idadi ya Wanachama kufikia 11,507, kutoka Wanachama 10,326 mwishoni mwa mwaka 2025.
Aidha, Bi. Mwakitalima alisema katika kipindi hicho Mali za Chama zimeongezeka na kufikia zaidi ya shilingi bilion 63, wakati akiba na amana za Wanachama zimefikia zaidi ya shilingi bilioni 50.
Mkutano Mkuu wa 13 wa Hazina Saccos umewakutanisha wawakilishi wa wananchama kutoka mafungu 432 na unafanyika ili kutoa fursa kwa wanachama kusimamia mweleo wa chama na wanachama kupokea taarifa ya utendaji, kutathmini maendeleo, kujadili changamoto na kufanya maamuzi yatakayoongoza mustakabali wa chama.








No comments:
Post a Comment