MSALATO YAFUNGUA AJIRA 9,059, UJENZI WA UWANJA WAFIKIA ASILIMIA 89 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 24, 2026

MSALATO YAFUNGUA AJIRA 9,059, UJENZI WA UWANJA WAFIKIA ASILIMIA 89



Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA


Jumla ya fursa za ajira 9,059 zimetolewa kwa Watanzania kupitia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma, huku ujenzi wa miundombinu ya uwanja huo ukifikia asilimia 89.02 na majengo asilimia 78.37 hadi Septemba 23, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Septemba 24, 2026 katika eneo la uwanja huo lililopo Msalato, jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema ajira hizo zimetolewa kupitia mikataba miwili mikuu ya utekelezaji wa mradi huo.

Amesema kandarasi ya ujenzi wa miundombinu (Package 1) imetoa ajira 3,571, huku kandarasi ya ujenzi wa majengo (Package 2) ikitoa ajira 5,488 kwa raia wa Tanzania.

Kwa upande wa miundombinu, Mhandisi Besta amesema baadhi ya kazi zimefikia hatua za juu za utekelezaji, ambapo njia ya kurukia na kutua ndege (runway) imefikia asilimia 98, njia za viungio (taxiways) asilimia 99, huku eneo la maegesho ya ndege (apron) likifikia asilimia 99.

Katika upande wa majengo, ujenzi wa Jengo la Abiria umefikia asilimia 81, Mnara wa Kuongozea Ndege asilimia 74, huku Kituo cha Zimamoto kikifikia asilimia 88.

Uwanja huo unajengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Daraja la 4E, ukiwa na njia ya kurukia na kutua ndege yenye urefu wa mita 3,600 na upana wa mita 45.

Utakapokamilika, uwanja huo unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia hadi abiria milioni 1.5 kwa mwaka, pamoja na kuwezesha kutua kwa ndege kubwa ikiwemo Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba hadi abiria 350.

Mhandisi Besta amesema kwa mujibu wa mpango wa ukamilishaji wa mradi huo, kazi za miundombinu zinatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 27, 2026, huku ujenzi wa majengo yote ukitarajiwa kukamilika Desemba 30, 2026.

Katika hatua nyingine, TANROADS imewataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) unaoashiria uwezekano wa mvua za El Niño katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026.

Mhandisi Besta amesema TANROADS itaendelea kuimarisha ukaguzi na matengenezo ya barabara, madaraja pamoja na mifumo ya maji, hatua inayolenga kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo na kulinda miundombinu nchini.






No comments:

Post a Comment