OMDTZ YAFANIKISHA MIPANGO YA KUKABILIANA NA MAFURIKO DAR ES SALAAM - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 22, 2026

OMDTZ YAFANIKISHA MIPANGO YA KUKABILIANA NA MAFURIKO DAR ES SALAAM




Na, mwandishi wetu - Dar es Salaam


Taasisi ya OpenMap Development Tanzania (OMDTZ), kwa kushirikiana na Serikali, imekamilisha zoezi la kukabidhi Mipango ya Maandalizi na Kukabiliana na Mafuriko kwa jamii katika kata tano za Jiji la Dar es Salaam.

Zoezi hilo limewezesha zaidi ya washiriki 1,345 kutoka katika kata za Keko, Mabibo, Ubungo, Makurumla na Tabata kupata mipango, elimu na taarifa muhimu za maandalizi na mwitikio wa mafuriko.

Aidha utekelezaji wa zoezi hilo umepitia Mradi wa “Ramani Zetu, Sauti Zetu”, unaofadhiliwa na Zayed Sustainability Prize, kwa lengo la kuhakikisha jamii na viongozi wa kata hizo wanakuwa na taarifa sahihi kuhusu maeneo yao ili kuwawezesha kujiandaa kabla ya mafuriko, kuchukua hatua wakati wa hatari na kuendelea kuwa salama baada ya tukio.




Katika kata hizo wananchi walipatiwa taarifa kuhusu maeneo hatarishi, njia salama za uhamishaji, maeneo ya mikusanyiko na maeneo yanayohitaji uangalizi zaidi wakati wa mafuriko.

Aidha, walipata elimu kuhusu hatua za kuchukua kabla na wakati wa mafuriko, matumizi ya Mifumo ya Tahadhari za Mapema, hatua za msingi za uokoaji na taarifa kuhusu mwenendo wa mvua za El Niño.

Akifunga rasmi zoezi hilo katika Kata ya Tabata, Diwani wa Kata hiyo, Mheshimiwa Masudi Masudi, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya jamii, viongozi na wadau katika kukabiliana na changamoto za mafuriko.

“Ushirikiano kati ya OMDTZ, viongozi na jamii umetusaidia kutambua changamoto na kuchukua hatua katika maeneo yetu. Mfano ni eneo la Mtaa wa Msimbazi Magharibi ambapo hatua zimechukuliwa na OMDTZ kwa kujenga mfereji wa kupokea maji. Tunahitaji kuendelea na ushirikiano huu ili kuhakikisha maandalizi yanaendelea kuwa sehemu ya maisha ya jamii,” amesema Mhe. Masudi

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa OpenMap Development Tanzania, Bw. Innocent Maholi, amesema kukamilika kwa zoezi hilo ni hatua muhimu katika kuhakikisha mipango na taarifa zilizotengenezwa kwa kushirikisha wananchi zinarejeshwa kwa jamii na kutumika katika kuchukua hatua.

Amehimiza viongozi na wananchi kuendelea kutumia zana zilizotolewa na OMDTZ katika shughuli za usafi wa mazingira, hususan usafishaji wa mifereji na maeneo yanayoweza kuziba na kusababisha maji kutuama.

"Mradi wa Ramani Zetu, Sauti Zetu unalenga kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya mafuriko kupitia matumizi ya ramani shirikishi, taarifa za jamii, mipango ya maandalizi na mwitikio wa maafa pamoja na uhamasishaji wa hatua za mapema," alisema Maholi

Aliongezea kuwa kupitia mradi huo, OMDTZ itaendelea katika Mikoa ya Pwani na Morogoro kushirikiana na Serikali na jamii katika kutumia taarifa za maeneo husika kuimarisha maandalizi, kupunguza vihatarishi na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mafuriko.




No comments:

Post a Comment