OSHA YAWAFIKIA WACHIMBAJI WADOGO NA ELIMU YA USALAMA, YAHIMIZA TAHADHARI DHIDI YA EL NINO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 25, 2026

OSHA YAWAFIKIA WACHIMBAJI WADOGO NA ELIMU YA USALAMA, YAHIMIZA TAHADHARI DHIDI YA EL NINO

Na Mwandishi wetu, Geita

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amewakumbusha wachimbaji wadogo mkoani Geita kuchukua tahadhari dhidi ya uwepo wa Mvua kubwa za El Nino zinazotarajia kunyesha hivi karibuni nchini.

Akifungua mafunzo ya Usalama na Afya kwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita, amesema kuwa ni vizuri wachimbaji hao kuchukua tahadhari mapema ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na uwepo wa mvua hizo.

"Niwatake wachimbaji wote kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kufuatilia taarifa za utabiri wa Hali ya Hewa toka Mamlaka ya Hali ya Hewa, ili kuchukua tahadhari mapema. Uchimbaji wetu ni wa "underground" hivyo, ni muhimu kujiridhisha kabla ya kuanza kufanya uchimbaji. Na endapo ikatokea madhara ya aina yoyote, basi ni vyema taarifa zitolewe mapema OSHA na Mamlaka zingine husika." alisema Mhe. Deus

Aidha, waziri huyo aliwakumbusha wachimbaji hao kutumia elimu walioipata na Vifaa Kinga vya mfano walivyopatiwa ili kuendelea kukumbushana umuhimu wa matumizi ya Vifaa Kinga na Kuchukua tahadhari.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema mafunzo hayo ni muendelezo na maelekezo ya mheshimiwa waziri katika kuyafikia makundi mbalimbali na kuyapatia elimu ikiwemo wachimbaji wadogo. Mafunzo kama hayo tayari yamekwishafanyika katika Wilaya za Bukombe na Namungo mkoani Lindi.

Bi. Mwenda amesema, wachimbaji wadogo wanakabiliwa na Vihatarishi vingi kutokana na aina ya uchimbaji wanaofanya, ndio maana OSHA iliamua kuyafikia makundi hayo na kuwapa elimu pamoja na kuwapatia PPE kwa lengo la kuhimiza matumizi ya Vifaa Kinga wakati wakitekeleza majukumu yao.

Washiriki wa mafunzo ambao wametoka katika mkoa wa Kimadini wa Mbogwe na Geita pamoja na wachimbaji toka nchi jirani ya Uganda, wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutambua na kuvidhibiti Vihatarishi sehemu za kazi pamoja na Huduma ya Kwanza.

Akizungumza kwa niaba ya Balozi wa Uganda nchini Tanzania, mwakilishi wa ubalozi huo, Brigedia Jenerali Julius Mbaine, amesema ushiriki wao katika maonesho hayo umefungua fursa ya kubadilishana uzoefu na kutambua maeneo ambayo Tanzania na Uganda zinaweza kushirikiana katika sekta ya madini.

“Sekta ya madini inatoa jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano. Ubalozi wa Uganda nchini Tanzania uko tayari kusaidia kuimarisha uhusiano wa kitaasisi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili, hususan katika kukuza uwekezaji, biashara na mnyororo wa thamani wa madini.” Amesisitiza Brigedia Jenerali Julius.

Amesema mazungumzo yaliyofanyika kati ya ujumbe wa Uganda na wadau wa madini Geita yamewapa nafasi ya kuelewa zaidi sekta hiyo nchini Tanzania na kutambua maeneo ya maslahi ya pamoja.

Ushiriki wa wachimbaji wadogo wa Uganda katika maonesho hayo unalenga kuwawezesha kujifunza kutoka kwa wadau wa Tanzania na kuona namna teknolojia na maarifa yanavyoweza kutumika kuboresha shughuli za uchimbaji.

Kwa Upande wake Mbunge wa Geita Mjini Mhe. Mha. Chacha Mwita Wambura, amepongeza juhudi za OSHA katika kuendelea kusimamia Usalama na Afya Mahali pa Kazi nchini. Amesema kuwa yeye kama mdau wa uchimbaji wa madini anatambua umuhimu wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi kutokana na maeneo hayo kuwa na vihatarishi.

Mafunzo ya Usalama na Afya kwa wachimbaji wadogo yameandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kushirikiana na mkoa wa Geita ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini, yanayofanyika Mkoani Geita.

No comments:

Post a Comment