LOWASSA APENDEKEZA MAMA TESHA KUTUNUKIWA TUZO YA HESHIMA YA RAIS - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 25, 2026

LOWASSA APENDEKEZA MAMA TESHA KUTUNUKIWA TUZO YA HESHIMA YA RAIS


Na Mwandishi Wetu - Arusha


Mbunge Mstaafu wa Monduli, Mheshimiwa Fredric Lowassa, ametoa wito kwa Tume inayomshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuzingatia mchango mkubwa wa Mwalimu Mama Tesha katika jamii na elimu, na kupendekeza jina lake kwa ajili ya kutunukiwa Tuzo ya Heshima ya Rais.

Mheshimiwa Lowassa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika Mahafali ya 27 ya Shule ya St. Margarets, mkoani Arusha, akieleza kuwa mchango wa Mama Tesha unapaswa kutambuliwa si katika sekta ya elimu pekee, bali pia kama mchango wenye umuhimu kwa taifa.

Amesema nchi nyingine, ikiwemo Uingereza, zina utaratibu wa kutambua watu waliofanya mchango mkubwa katika jamii kupitia tuzo za heshima, akitumia uzoefu wake akiwa Mbunge wa Monduli kueleza namna alivyowahi kusaidia mgeni mmoja aliyekuwa ametoa mchango katika mradi wa maendeleo Meserani kupata tuzo kama hiyo.

“Nikiwa Mbunge wa Monduli, alikuja Mzungu mmoja alitusaidia mradi pale Meserani. Akaniambia nimwandikie barua kwenda kwa Malkia wakati ule, ili nimwombe apate tuzo ya heshima. Na nilimwandikia kutoka Monduli kwa sababu mchango huo alitusaidia Monduli, alipata ile tuzo ya heshima,” amesema Lowassa.

Akihusisha uzoefu huo na mchango wa Mama Tesha, Mheshimiwa Lowassa amesema sasa ni wakati muafaka kwa Tanzania kuwa na utaratibu wa kutambua watu walioleta mafanikio makubwa katika jamii, akisisitiza kuwa Mama Tesha anastahili kupewa heshima hiyo kutokana na mchango wake.

“Ninasema na nitatoa wito leo kwa Tume ambayo inamshauri Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sasa ni wakati muafaka na sisi kama taifa tukaweza kutambua mafanikio makubwa kama ya Mwalimu Mama Tesha, akatambuliwa akapokea tuzo ya heshima ya Mheshimiwa Rais kwa mchango wake huo,” amesema.

Mheshimiwa Lowassa ameongeza kuwa suala la kutambua watu wenye mchango mkubwa linapaswa kuwa la kitaifa na kugusa sekta mbalimbali, akisema pendekezo la Mama Tesha ni hatua ya kuanzia katika kutambua mchango wa watu waliotoa huduma kubwa kwa jamii.

“Ni wakati sasa wote tukumbushane, wote ni jambo la kitaifa, sisemi sekta ya elimu pekee lakini kila sekta. Lakini sisi tunaanza kwa kupendekeza jina la Mama Tesha litambuliwe, lipate tuzo ya heshima ya elimu ya taifa kwa ujumla,” amesema.

Kauli hiyo imekuja ikiwa sehemu ya hotuba yake katika Mahafali ya 27 ya Shule ya St. Margarets, ambapo amesisitiza umuhimu wa jamii na taifa kutambua mchango wa watu wanaojitoa katika kujenga na kuendeleza jamii.

No comments:

Post a Comment