WATOTO MILIONI 8.5 HATARINI KUTOFIKIA UWEZO WAO TIMILIFU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 25, 2026

WATOTO MILIONI 8.5 HATARINI KUTOFIKIA UWEZO WAO TIMILIFU


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Serikali imesema takribani watoto milioni 8.5 nchini Tanzania wako katika hatari ya kutofikia ukuaji wao timilifu kutokana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.


Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Profesa Tumaini Nagu, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, wakati akifunga mkutano wa nusu mwaka wa tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, uliofanyika jijini Dodoma.


Profesa Nagu amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na watoto takribani milioni 16, sawa na asilimia 27 ya Watanzania wote, huku matokeo ya Utafiti wa TDHS-MIS wa mwaka 2022 yakionyesha kuwa asilimia 53 ya watoto wenye umri wa miaka miwili hadi minne wako katika hatari ya kutofikia ukuaji wao timilifu.


Amesema hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na umaskini, kiwango duni cha elimu, makazi yasiyokidhi mahitaji pamoja na upatikanaji hafifu wa huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.


Kwa mujibu wa Profesa Nagu, athari za kutofikia ukuaji timilifu haziishii katika kipindi cha utoto, bali zinaweza kuendelea hadi mtoto anapofikia utu uzima na kuathiri uwezo wake wa kiuchumi.


Amesema tafiti zinaonyesha kuwa watoto wanaokabiliwa na changamoto hizo wanaweza kupata wastani mdogo wa kipato wanapokuwa watu wazima, hali inayoweza kuchangia kushuka kwa hali ya uchumi wa familia na kuendeleza mzunguko wa umaskini.


Profesa Nagu amesema uwekezaji katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto una manufaa makubwa kiuchumi, akirejea utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa mwaka 2018 unaoonyesha kuwa kila dola moja ya Marekani inayowekezwa katika hatua jumuishi za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto inaweza kuzalisha hadi dola 17.


“Kutokana na matokeo hayo, hatuna budi kuweka na kutekeleza mikakati thabiti ya kuimarisha huduma bora za malezi kwa watoto kuanzia ngazi ya familia, jamii na katika taasisi mbalimbali,” amesema.


Amesisitiza kuwa msingi wa malezi bora huanzia katika familia, akieleza kuwa ushirikiano wa wazazi wote wawili ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata mazingira yanayowawezesha kukua na kufikia uwezo wao.


Katika hatua nyingine, Profesa Nagu amesema Serikali, kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo, imepata mafanikio mbalimbali katika utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.


Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuongezeka kwa usajili wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana kutoka vituo 2,378 mwaka 2024 hadi vituo 5,963.


Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto wenye ulemavu na mahitaji maalumu wanajumuishwa katika mipango na shughuli mbalimbali za maendeleo, huku akitaka bajeti maalumu itengwe kwa ajili ya upatikanaji wa vifaa saidizi kulingana na mahitaji yao.


“Ni vyema watu wenye ulemavu kutengewa bajeti itakayosaidia katika ununuzi wa vifaa, ikiwemo mafuta kwa wenye ulemavu wa ngozi, vifaa vya kutembelea (wheelchair) na mahitaji mengine muhimu,” amesema.


Vilevile, Profesa Nagu ameiagiza mikoa kuhakikisha watoto wote wanaohudhuria vituo vya kulelea watoto wadogo mchana wanasajiliwa katika Mfumo wa Taarifa za Shule (School Information System).


“Mikoa isimamie na kuhakikisha watoto wote walioko kwenye vituo vya kulelea watoto wadogo mchana wanasajiliwa kwenye mfumo wa taarifa za shule. Naliwekea msisitizo suala hili kwa kuwa bado mikoa yote haijafanya vizuri katika eneo hili,” amesema.


Pia amevitaka vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kuanzisha sehemu maalumu za kutolea huduma za malezi na maendeleo ya awali ya mtoto, maarufu kama ECD Corner, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.



Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Felister Mdemu, amesema utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 unahitaji hatua thabiti na uwekezaji mkubwa katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.


Amesema uwekezaji huo ni sehemu muhimu ya kujenga kizazi chenye afya, uwezo wa kujifunza, maadili mema, ustahimilivu na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.


“Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa juhudi tunazofanya leo zinajenga kizazi chenye afya, uwezo wa kujifunza, maadili mema, ustahimilivu na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa letu,” amesema Mdemu.


Mdemu pia amezitaka taasisi zote zinazohusika na programu hiyo kufanya vikao vya ndani vya kujipanga upya, kupitia wajibu wao katika utekelezaji wa MMMMAM na kuweka hatua mahsusi za utekelezaji kwa muda mfupi na wa kati.


Amesema mafanikio ya ushirikiano katika programu hiyo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya mikutano inayofanyika, bali kwa idadi ya watoto wanaofikiwa, ubora wa huduma wanazopata, usalama wa mazingira wanamoishi na maendeleo wanayoyapata.




No comments:

Post a Comment