PROF. SHEMDOE AELEKEZA MAJIJI KUWA NA KAMPENI MAALUM YA WIKI MBILI YA USAFI WA MAZINGIRA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 8, 2026

PROF. SHEMDOE AELEKEZA MAJIJI KUWA NA KAMPENI MAALUM YA WIKI MBILI YA USAFI WA MAZINGIRA


Na. OWM – TAMISEMI, Dodoma


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Prof. Riziki Shemdoe amewataka viongozi wa mikoa yenye majiji, viongozi wa majiji na manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha wanatekeleza kampeni maalum ya wiki mbili ya usafi wa mazingira katika majiji, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha usafi wa mazingira katika majiji aliyoyatoa Septemba 02, 2026 wakati akiwaapishwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala aliowateua Agosti 27, 2026.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo Septemba 07, 2026 wakati wa Kikao kazi chake na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Dodoma, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Tanga, Wakuu wa Wilaya zenye Majiji, Wastahiki Meya wa Majiji, Wakurugenzi wa Majiji pamoja na Wakurugenzi wa Manispaa za Dar es Salaam.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amezielekeza Halmashauri zote nchini kuandaa mpango wa namna ya kushughulikia ukusanyaji na uchakataji wa taka ngumu na taka tope zikihusishaa majiji na manispaa na kuongeza kuwa ziwasilishe mipango hiyo ofisini kwake.

Aidha, Prof. Shemdoe amezitaka halmashauri zote kwa kushiirikiana na Baraza la Mazingira (NEMC ) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuchukua hatua ya kutatua changamoto ya kelele zinazotokana na uwepo wa kumbi za starehe jijini Dar es salam, akitoa mfano wa ukubwa wa changamoto hiyo katika Manispaa ya Kinondoni.

Akizungumzia ujenzi wa miundombinu ya kudumu kwenye maeneo ya wazi, Prof. Shemdoe amewataka Wakuu wa Mikoa kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi kwenda kufanya mapitio upya ya maeneo ya wazi yaliyotolewa na Serikali lakini yanajengwa miundombinu ya kudumu, na kuongeza kuwa ofisi yake haitolifumbia macho suala hilo iwapo halitatekelezwa kikamilifu.

Pia, ameilekeza Manispaa ya Kinondoni kuweka mkakati wa kusitisha biashara za machinga katika maeneo yasiyo rasmi, na kuutaka uongozi wa manispaa hiyo kuwatafutia wafanyabiashara sehemu rasmi za kuendesha shughuli zao.  

Ili kukabiliana na changamoto ya uzalishaji kelele, Prof. Shemdoe amewataka Wakuu wa Mikoa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na Wakuu wa Polisi wa Mikoa (RPC) kukabiliana na wamiliki wa vyombo vya usafiri hasa magari na pikipiki ambao hutoa mabomba ya moshi (exhaust) katika vyombo vyao na kusababisha kelele katika jamii.

Kutokana na umuhimu wa usafi wa mazingira, Prof. Shemdoe ameelekeza ajenda ya usafi wa mazingira iwe ya kudumu kwenye vikao vya ngazi zote kuanzia mikutano ya vijiji, Kata , Mabaraza, Kamati za Ushauri za Mikoa (RCC), Kamati za Ushauri za Wilaya (DCC) na vikao vingine vya kiofisi.

Ili kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa maelekezo yake, Prof. Shemdoe amemuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuandaa kipimo cha utendaji (KPI) kwa ajili ya ufuatiliaji na kuwezesha kushindanisha halmashauri, manispaa na majiji kwenye eneo la usafi wa mazingira.

Akihitimisha kikao kazi hicho, Prof. Shemdoe amewataka viongozi hao kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa maelekezo yote aliyoyatoa baada ya wiki mbili za utekelezaji.

No comments:

Post a Comment