QWARAY AWATAKA WAAJIRI KUZINGATIA SHERIA ILI KULINDA HAKI ZA WATUMISHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, September 7, 2026

QWARAY AWATAKA WAAJIRI KUZINGATIA SHERIA ILI KULINDA HAKI ZA WATUMISHI





Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray, amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanawaongoza na kuwasimamia ipasavyo watumishi walio chini yao ili kuondoa changamoto zinazoweza kuwanyima haki zao za msingi, ikiwemo kupanda vyeo, na hivyo kulinda morali ya kazi na kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma.

Mhe. Qwaray ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati alipotembelea Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kukagua zoezi la ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria za utumishi wa umma linalofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.

Amesema waajiri wana wajibu wa kuhakikisha watumishi wanafahamu majukumu yao, wanapata usimamizi unaostahili na wanatekeleza kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma.


Mhe. Qwaray amesema ukaguzi unaoendelea umebaini changamoto katika matumizi ya mfumo wa PEPMIS, hali ambayo imewafanya baadhi ya watumishi kushindwa kufikisha alama 75 zinazohitajika ili kuwa na sifa za kupanda vyeo.

Amesema baadhi ya watumishi wamekuwa wakiondoa majukumu kwenye mfumo bila kuwashirikisha au kuwataarifu wasimamizi wao, huku baadhi ya wasimamizi wakishindwa kuidhinisha utekelezaji wa majukumu hayo.

“Hakuna haki bila wajibu,” amesema Mhe. Qwaray, akiwataka watumishi wa umma kuzingatia maadili, uadilifu na viapo walivyokula katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhe. Qwaray ameipongeza Tume ya Utumishi wa Umma kwa kujenga mfumo wa kielektroniki wa ukaguzi, akisema matumizi ya teknolojia yanaifanya Serikali kuwa ya kisasa na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.

Amezitaka taasisi zote za umma ambazo bado hazijajiunga na mifumo ya e-Watumishi na e-Utendaji kufanya hivyo kwa haraka ili kurahisisha usimamizi wa watumishi na utoaji wa huduma.

Amesema Serikali imewekeza takribani Shilingi bilioni 1.4 katika kuimarisha mifumo ya kielektroniki kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi na kupunguza malalamiko katika utumishi wa umma.


Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Hamisa Kalombola, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Tume kupata bajeti iliyowezesha ujenzi wa mifumo ya kielektroniki.

Jaji Kalombola amesema mifumo hiyo imeongeza kasi, urahisi na tija katika utendaji kazi wa Tume, pamoja na kuimarisha utoaji wa haki kwa watumishi wa umma.

Amesema Tume itaendelea kutumia mamlaka yake kuhakikisha mamlaka zote za ajira na nidhamu nchini zinatekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Pia amemshukuru Mhe. Qwaray kwa kuungana na Tume katika zoezi la ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria za utumishi wa umma kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Kwa upande wake, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Ndugu Nolasco Kipanda, amesema Tume hiyo ina majukumu makuu matatu ambayo ni kutoa ushauri, urekebu na usimamizi, pamoja na utoaji wa haki kwa watumishi na waajiri.

Amesema Tume imetuma timu 15 katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria za utumishi wa umma.

Hadi sasa, zaidi ya taasisi 60 za umma zimekaguliwa, huku kila timu ikiwa na mpango wa kukagua taasisi tano katika kila kituo.

Zoezi hilo lilizinduliwa Agosti 10, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, na linafanyika katika mikoa 16 nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Msaji wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Martin Rugorabamu amesema kuwa hadi Juni 30, 2026, jumla ya wahandisi 33,046 wamesajiliwa nchini katika ngazi mbalimbali.

Kati yao, wahandisi wanawake ni 6,490, huku makandarasi wasaidizi (Technicians) wakiwa 3,762.

ERB pia imesajili makampuni ya ushauri wa kihandisi ya ndani 331 na ya nje 105, pamoja na maabara 56 za upimaji wa vifaa vya ujenzi.

Katika mwaka wa fedha 2025/2026, ERB ilipanga kukagua miradi 600, lakini ilifanikiwa kukagua miradi 791 ya majengo, barabara, maji, umeme na viwanda.

Bodi pia ilisajili miradi 1,540 kati ya 1,500 iliyopangwa, ikatoa leseni 10,605 na kuwaapisha wahandisi 1,356.








No comments:

Post a Comment